Dar
es Salaam. Timu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara
imepanga kubadili jezi zao wanazozitumia zenye rangi ya zambarau na
nyeupe ndani ya mwaka huu.
Mbeya City ambayo imepanda daraja msimu huu,
imeonekana kuwa tishio kwa klabu kongwe nchini za Simba na Yanga
kutokana na upinzani mkubwa wanaoutoa katika Ligi Kuu inayoendelea
nchini.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa timu
hiyo, Mussa Mapunda alisema kuwa lengo kubwa ni kubadilisha jezi hizo
ili ziwe na mwonekano tofauti kati ya wachezaji na mashabiki
wanaoishangilia Mbeya City ndani ya Tanzania na mpakani mwa Malawi na
Zambia. Alisema soko la jezi zao hivi sasa limeongezeka tofauti na
mwanzoni wakati timu yao inapanda kutoka daraja la kwanza kwenda Ligi
Kuu, hivyo wamepanga kuzindua rasmi jezi mpya za Mbeya City ndani ya
mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Aliongeza kuwa, wamepanga kuleta kontena zima la
jezi likiwa pamoja na bendera, kofia, skafu, soksi zenye rangi ya
zambarau na nyeupe zinazoiwakilisha timu hiyo.
“Baada ya soko la jezi kuongeza kwa kasi kubwa
ndani na nje ya nchi, hivi sasa tumeona ni bora tubadili muonekano wa
jezi ya timu yetu, tunataka jezi za wachezaji na mashabiki zitofautiane
kidogo.
“Mpango huo tumepanga kuuanza ndani ya mwaka huu,
uzinduzi wake utafanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, tayari tumeanza
mazungumzo na mawakala wetu wanaotutengenezea jezi waishio nchini
China,”alisema Mapunda.
|