skip to main |
skip to sidebar
HABARI KAMILI KUHUSU MBWA ALIYEKUTWA NA MGUU WA MTU MKOANI MBEYA
IMANI
za kishirikina zimezidi kukitisa Kijiji cha Isange, Kata ya Isange,
Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya baada ya matukio ya kupotea na kuuawa kwa
watoto kutokea mara kwa mara ambapo safari hii binti mmoja wa darasa la
saba ameuawa na mguu wake kukutwa ukiliwa na mbwa.
Binti huyo
aliyeuawa amegundulika kuwa ni mwanafunzi wa darasa la saba
aliyejulikana kwa jina la Lista Sebule aliyekuwa akisoma katika Shule ya
Msingi Mpombo iliyopo Isange na alipotea katika mazingira ya
kutatanisha na maiti yake kukutwa kando ya mto siku tisa baadaye. Katika
tukio la awali, mtoto mmoja alikatwa kichwa na watu wasiojulikana kisha
kutoweka nacho.
Mama mzazi wa marehemu, Christina Sakalile alisema
binti yake (Lista) alipotea saa tisa jioni ya Machi 31, mwaka huu baada
ya kutumwa kupeleka simu kibandani ili ‘ikachajiwe’ lakini hakurudi hadi
giza lilipoingia, hali iliyozua wasiwasi na wakaanza kumtafuta bila
mafanikio.
“Baada ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isange,
Daudi Nsyani aliitisha mkutano wa wananchi wote ili mtoto atafutwe.
Juhudi hizo zilizaa matunda Aprili nane, mwaka huu lakini alipatikana
akiwa amekufa huku akiwa hana baadhi ya viungo mwilini,” alisema mama
huyo huku akitokwa machozi.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema mwili
wa marehemu ulipatikana ukiwa kando ya Mto Nkalisi uliopo kijijini hapo
ukiwa umekatwa kichwa na miguu ambapo mguu mmoja ulipatikana baada ya
mbwa kukutwa akiwa anaula na alipoona watu akawa anakimbia nao.
Hali
hiyo iliwafanya watu kumfuatilia mbwa huyo ambaye aliongoza hadi kwenye
mwili wa marehemu na kuwakuta mbwa wengine wawili wakiwa kando yake
ambapo uongozi wa kijiji uliliarifu jeshi la polisi.
“Polisi
walipofika walifanya uchunguzi na wananchi wakapiga kura ya siri ambapo
watu wawili walikamatwa wakituhumiwa kuhusika na tukio hili. Mwili
ulikabidhiwa kwa ndugu na wakauzika siku hiyohiyo na mazishi yake
yaliweka historia kwa kuhudhuriwa na watu wengi,” alisema shuhuda huyo.
Diwani wa Kata ya Isange, Elias Mwandele amethibitisha kutokea tukio
hilo na aliwataka wazazi kutowapeleka watoto kwenye shughuli za kuchunga
mifugo kwa sasa. (Habari, picha na Mbeya Yetu)