MAMLAKA ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma nchini (VETA), imezindua
kitabu maalum kitakachotumika katika kutoa mafunzo kwa madereva nchini
kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani na matukio mengine.
Mkuu wa Chuo cha Veta Chang’ombe, Samuel Ng’andu anasema kuwa chuo
chake kimeandika kitabu hicho ili kitumiwe na vijana wanaojiunga na
mafunzo ya udereva pamoja na wadau wengine wa usafirishaji nchini, ili
waweze kujua mambo ya msingi hasa ya kisheria yahusuyo taaluma ya
usafirishaji wa abiria na vyombo vyake.
Anasema kitabu hicho kilichozinduliwa jijini Mwanza hivi karibuni na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, kina mada za alama za
usalama barabarani, vimiminika sahihi vinavyotumika kwenye vyombo vya
moto na taarifa mbalimbali zilizo kwenye tairi la gari.
“Mada zilizowekwa ni zile ambazo bado watumiaji wa magari wanazipuuza
wanapokuwa barabarani ama wanapotakiwa kufanya matengenezo madogo
madogo kwenye magari yao,” anasema. Anaamini kitabu hicho kinaweza kuwa
na mapungufu kwenye baadhi ya sehemu, lakini anatoa mwito kwa watumiaji
wasisite kuwapatia mrejesho ili waweze kukifanyia marekebisho zaidi siku
zijazo.
“Tumeandika kitabu hiki, kutokana na kuguswa sana na tatizo la ajali
zinazoendelea kutokea hapa nchini, kila siku watu wakiwemo wataalamu wa
kada tofauti hufariki dunia, sio kwamba wanakwenda na kurudi, hapana
hawawezi kurudi, inatia uchungu sana,” anafafanua.
Kitabu hicho chenye rangi ya njano, iking’arishwa na picha za magari
na mabasi kwa jarida la juu, na picha inayoonesha majengo ya Chuo cha
Veta, Chang’ombe kwa jarida la nyuma, kina jumla ya kurasa 33. Anasema
kitabu hicho kimechapishwa na wataalamu wa Veta Chang’ombe kwa
kushirikiana na Polisi kupitia kitengo cha uchapishaji ili kiweze
kuisaidia jamii kujikomboa kifikira kwa kuondokana na tatizo la ajali,
ili siku moja ibaki historia kwa vizazi vijavyo.
Anasema jamii ikizingatia machapisho ya usalama barabarani kwa
kuyasoma kwa umakini, na kuyatekeleza kwa vitendo, vita ya ajali za
barabarani itakuwa rahisi.
“Sote tutakuwa mashahidi wa kushuhudia ushindi, dhidi ya adui wa
taifa hili, ‘ajali za barabarani’,” anasema. Anasema hatua ya Veta
kutunga kitabu hicho inaonesha kuwa wafanyakazi wake wameanza kuitikia
mwito wa viongozi wao wa kujitoa kuandika vitabu vinavyoendana na
taaluma zao.
“Veta inaamini kuwa walimu wanapoandika vitabu vinavyoendana na
mitaala ya kufundisha, vitawafanya wahitimu wetu kukubalika kwenye soko
la ajira kwa kuajiriwa na kujiajiri wenyewe kwani vitabu hivi huandikwa
kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na tafiti
mbalimbali,” anaeleza na kuongeza kuwa kitabu hicho kimekamilika kwa
usimamizi bora uliofanywa na yeye mwenyewe.
Anasema hatua ya uandishi wa vitabu, imetokana na Veta kujiwekea
utaratibu wa kuwapeleka wafanyakazi wake viwandani kupata ujuzi na
maarifa mapya juu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa sekta zote,
ikiwemo ya udereva.
“Tunawapongeza wafanyakazi wetu , walio tayari kutumia muda wao
kuandika vitabu ili taifa letu siku moja liongeze kasi ya maendeleo
katika kupambana na ajali,” anasema. Analishukuru Jeshi la Polisi
nchini, Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kutoa changamoto mbalimbali
ili taasisi zinazoendesha mafunzo ya udereva ziweze kuandika vitabu
mbalimbali vya elimu ya udereva.
“Tunaishukuru Kampuni ya BP kwa kuturuhusu kutumia kipeperushi
kinachoelezea mojawapo ya kundi la oili kwa gari za kisasa na za zamani
na bila ya kumsahau mtungaji wa kitabu cha usalama barabarani kwa
makundi ya watu maalum,” anasema na kuwataja walioshirikiana kuandaa
kitabu kuwa ni Kisembe Kapele ambaye ni Mkufunzi Mkuu, Mratibu wa
Mafunzo Mashaka Kassara, Mkufunzi Msaidizi David Kwegela na Muongozaji
Mafunzo ya Udereva, Kigalu Sawaka, wote wakiwa ni kutoka Shule ya
Mafunzo ya Udereva ya jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Lwenge aliwashukuru Veta kwa uamuzi
wao wa kutunga kitabu hicho, ambacho anasema kitajenga uelewa mpana kwa
jamii na hivyo kuifanya nchi kuwa na uwezekano mkubwa wa kuzuia ajali.
“Niwashukuru kwa uamuzi wenu wa kuandika kitabu hiki, ambacho
kitakuwa ni dira muhimu kwa watumiaji wetu wa barabara, rai yangu kwa
wananchi na madereva naomba watumie sehemu ya muda wao ili waweze
kukisoma na kujifunza mambo ya msingi,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Mhandisi Moshi Zebania anasema Veta imetunga
kitabu hicho ili kusaidia taifa lijikomboe kifikra katika tatizo sugu
la ajali. “Naomba wananchi wakisome kitabu hiki, na tunayo imani kuwa
kitakuwa msaada kwa taifa, maana kinafafanua juu ya vimiminika
vitumikavyo kwenye magari, magurumu ya magari na mawasiliano wakati
dereva anapoendesha gari,” anasema.
Maudhui ya kitabu Kitabu hicho katika ukurasa wake wa kwanza,
kinaelezea alama za barabarani, jinsi mtumiaji wa barabara anavyopaswa
kutumia alama hizo wakati wa kuendesha gari lake. Mtunzi wa kitabu hicho
ambaye katika makala haya atatambuliwa kama Veta kupitia kwa Mkuu wa
Chuo cha Chang’ombe, Samuel Ng’andu, anasema mtu hawezi kuwa mchungaji
wa kanisa au imamu wa msikiti bila ya kujua Biblia au Quran.
Anaamini kwamba mchungaji au imamu huwaongoza waumini wao kwa kutumia
vitabu vya imani zao na sio kwa akili zao. Anasema mtu kujua kuendesha
gari kitaalamu ni pamoja na kujua tafsiri sahihi za alama zote, kuzitii
na kuziheshimu maana alama ni mwongozo kwa watumia barabara wote nchini.
Anasema alama ni chombo au mashine au rangi iliyopakwa au kutokupakwa
ili kuweza kutoa picha au ujumbe wa mazingira ya eneo alipo mtumiaji wa
barabara.
Ujumbe huo unaweza kuwa ni kiwango cha mwendo wa juu kinachoruhusiwa
katika barabara husika, ama sehemu ambayo dereva anatakiwa kuwaacha
watumiaji wengine wa barabara wavuke kwanza na ni maeneo ambayo mtumiaji
hupata huduma zingine, kama vile za mafuta ya petroli au dizeli.
Anasisitiza kuwa mtu hawezi kuwa dereva bila ya kuwa mahiri kwenye
tafsiri sahihi za alama za michoro ya barabarani na kuzitekeleza kwa
wakati mwafaka.
Ukurasa wa 2 hadi wa 15, mtunzi anaelezea umuhimu wa lugha ya makundi
ya alama za barabarani, ambapo anazitaja baadhi ya alama za makundi
hayo kuwa ni alama za onyo na tahadhari, alama ya amri (amri
zinazokataza na kulazimisha), alama za taarifa na maelekezo na alama za
usuli wa michoro ya barabarani.
Alama za usuli, hutoa tafsiri kadhaa zikiwemo zile zinazoonesha
barabara kufungwa, ambapo rangi ya njano na nyeusi hutumika kuonesha
kwamba barabara imefungwa kwa muda. Zipo pia alama za rangi nyekundu na
nyeupe ambazo huonesha barabara kufungwa moja kwa moja na hivyo haiwezi
kutumiwa na vyombo vya usafiri.
Alama zingine ni zile zinazoonesha dereva kutakiwa kupinda kulia au
kushoto, zinazoonysha kona kali iliyo kwenye barabara husika na
nyinginezo nyingi. Msomaji anashauriwa kununua kitabu hicho ambacho
kinauzwa kwa Sh 7,000 na kinapatikana katika vyuo vya Veta vilivyo
kwenye kanda zote na mikoa nchini.
Jambo zuri katika kitabu hicho alama zote zimeorodheshwa na kuwekewa
tafsiri yake, jambo ambalo litamuwezesha msomaji kukisoma kitabu hicho
na kukielewa vizuri. Ukurasa wa 16 wa kitabu hicho, mtunzi anawaonesha
askari wa Usalama Barabarani, wanavyotakiwa kutoa amri kwa watumiaji wa
barabara, ambapo ishara mbalimbali kuhusiana na maaskari wanavyotakiwa
kusimama na kutoa amri hizo zimefafanuliwa katika kitabu hicho.
Ukurasa wa 17 mtunzi anaelezea juu ya alama za barabarani, onyo na
taarifa kwa makundi maalum zinazokwenda sanjari na tafsiri za alama za
taarifa kwa makundi maalum.
Makundi hayo ni ya watu wa ulemavu tofauti tofauti katika jamii. Kwa
mfano, mtunzi anaonesha katika alama hizo kuwa mbele kuna kivuko cha
walemavu wa macho, ama rangi ya fimbo inayotumiwa na walemavu wa macho
mara kwa mara huwa ni ya rangi nyeupe.
Maelezo mengine aliyoeleza mtunzi ni utunzaji wa gari, usafishaji
wake, uwekaji wa vilainishi muhimu vinavyohitajika na kiwango cha joto.
Pia kuna taasisi zinazojihusisha na kuangalia ubora wa oili, ambapo hapa
dereva anashauriwa kuwa na utaratibu wa kutumia oili yenye mchanganyiko
wa hali ya hewa.
Mengine ni vigezo vya kuangalia wakati wa kununua oili, namna ya
kutumia mafuta ya breki, muda wa kufanya kazi kwa magurudumu, ambapo
dereva anashauriwa kutumia aina ya mafuta ya breki yaliyopendekezwa na
mtengenezaji wa gari kama ambavyo husomeka kwenye mfuniko wa mtungi wa
mafuta ya breki!
Mtunzi anahitimisha kwa kumtaka, dereva aendeshe gari lake kwa
kuzingatia taarifa zilizopo kwenye tairi, asibebe mzigo kupita kiasi,
asiweke tairi lililo na mwendokasi tofauti na mwendokasi unaozalishwa
kwenye injini, tairi lisilo kuwa na uwezo wa kuhimili matope kwenye
barabara za tope nyakati za mvua.
Ni imani kwa watu wengi kwamba madereva wa pikipiki wataacha ubahili
na kuwa wa kwanza kununua kitabu hiki kwani wengi wanaendesha bila kujua
ama kufuata kanuni za usalama barabarani. Imani pia ni kwamba, kwa vile
elimu haina mwisho, hata madereva ambao tayari wamepita vyuoni na wako
barabarani watachangamkia kitabu hiki ili kujenga utamaduni wa
kujikumbusha kile walichojifunza mara kwa mara.