MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Dk Pindi
Chana amewaomba wabunge, wahariri na wadau wa masuala ya habari nchini
kumpa majibu nini kifanyike pale magazeti yanapotumika kuchochea mambo
kwa kuandika habari za kupendelea upande mmoja, au za kuvuruga amani.
Dk Pindi alisema hayo jana bungeni
wakati akichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa mwaka 2013, uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Jaji Frederick Werema, ambao ndani yake kuna sheria tofauti 14
zinazofanyiwa marekebisho, ikiwemo Sheria ya Magazeti ya 1976.
Katika mchango wake huo, Dk Pindi ambaye
ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala,iliyoshughulikia muswada huo, alitoa ombi hilo kwa maelezo kuwa
yeye hana majibu.
“Wametuambia lengo la marekebisho ya
Sheria hii ya magazeti ni kuongeza adhabu, ili kulinda matumizi ya lugha
ya matusi yanayoweza kusababisha ukosefu wa amani, sasa nauliza pale
ambapo magazeti yanatumika kuchochea mambo na kuvunja amani, ndio uhuru
wa habari, nauliza na sina majibu, wahariri , wabunge niambieni,"
alihoji Dk Pindi.
Alisema hana matatizo na vyombo vya
habari, wala waandishi au wahariri, lakini wapo baadhi yao wananunuliwa
na kikundi cha watu kupotosha ukweli au kupendelea upande fulani, na
kuhoji wachache hao wafanyweje?
“Wale wanaotumika ndivyo sivyo, leo
Bunge hili liseme nini kifanyike, Watanzania wenzangu tusaidiane pale
ambapo kikundi cha watu kinatumia vyombo vya habari kubeba kikundi
kimoja na hususan kwa wanasiasa (magazeti) yanatumika sana tufanyeje?”
aliendelea kuhoji Dk Pindi.
Akitoa mfano alisema kuna nchi leo
zinashindwa kurudisha amani, na kuitaja nchi ya Misri kuwa wameshindwa
kurudisha amani yao na kutaka Watanzania na wadau nchini kusaidiana
kupata jibu ya swali hilo.
Akitoa mfano alisema kichwa cha habari
kinapoandikwa kwamba mtu fulani ni jangili, alafu kesho akaombwa radhi,
ili hali hata Mahakama haijathibitisha mashitaka yaliyoandikwa dhidi ya
mtu huyo, na kusema hali hiyo inamshushia heshima mtuhumiwa.
“Magazeti yanapaswa kuelimisha umma na kuwafundisha lakini vichwa vya habari hivi leo vinaandika nini?" alihoji Dk Pindi.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Muhagama
(CCM), aliitaka Serikali kuleta Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari
ili ujadiliwe bungeni, kwani ndio suluhu na ukombozi wa vyombo vya
habari. “Serikali yangu tuleteeni Muswada huo, Kamati ya Maendeleo ya
Jamii inalia huko, kwa nini tunachelewa kuuleta?Uletwe ili Bunge
liujadili na kuupitisha tupate sheria itakayolinda tasnia yote na
kuangalia weledi,” alisema Muhagama.
Alisema kuna watu wanaidhalilisha tasnia
ya habari bila sababu na kuitaka Serikali ilete Muswada huo ili itoe
majibu ya maswali yanayoulizwa kila kukicha ya magazeti nchini.
“Ukiletwa hapa tutaujadili na tutapata
sheria nzuri ya kuangalia vyombo hivi, na kuhakikisha amani ya taifa
hili inalindwa, uleteni hapa tuujadili,” alisema Mhagama.
Kambi ya Upinzani Bungeni katika hotuba
yao iliyosomwa na Msemaji wao,Tundu Lissu, imeitaka Serikali kufuta
kabisa Sheria ya Magazeti ya sasa na badala yake, ilete Muswada bungeni
utakaotunga sheria mpya itakayohifadhi uhuru wa habari na uhuru wa
mawazo.
Lissu alisema hiyo inatokana na ukweli
kwamba kuna madai ya msingi ya muda mrefu yaliyotolewa Mwaka 1991 na
Tume ya Nyalali ikitoa mapendekezo kwa Serikali kuleta Sheria ya Uhuru
wa Magazeti, kwani sheria zilizopo hazitoi uhuru huo.
Awali akiwasilisha marekebisho ya sheria
hiyo, Jaji Werema alisema katika sheria hiyo vifungu vinavyofanyiwa
marekebisho ni kile cha 36(1) na 37 (1) (a).
Sheria hiyo kwa sasa kabla ya
marekebisho kuletwa bungeni, kifungu cha 36 (1), kinasomeka; “ mtu
yeyote atakayechapisha habari za uongo, au za uzushi au kuchapisha
taarifa itakayosababisha woga na kuleta uchochezi katika jamii au kuleta
usumbufu, utakaondoa hali ya amani, atakuwa amepatikana na hatia ya
kutenda kosa na atakabiliwa na adhabu ya kulipa faini isiyozidi Sh
150,000. Au kwenda jela kwa miaka isiyozidi mitatu au kutumikia adhabu
zote kwa pamoja.”
Baada ya marekebisho, sheria hiyo
imeongeza adhabu ya faini hadi kufika Sh milioni tano. Kadhalika,
kifungu cha 37 (1) b, kinachohusu uchochezi kwa lengo la kusababisha
vurugu, na kuharibu mali, wahusika watakabiliwa na makosa ya kulipa
faini ya Sh milioni tano au kwenye jela kwa miaka mitatu au kutumikia
adhabu zote kwa pamoja.
Akiwasilisha marekebisho kwenye sheria
hiyo, Jaji Werema alisema lengo ni kuongeza adhabu ya faini kwa makosa
ya kutumia lugha za matusi na uchochezi zinazoweza kusababisha machafuko
nchini.