Newala. Katika Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara
lipo shimo la ajabu lijulikanalo kama ‘Shimo la Mungu’ lililochukua robo
tatu ya ukubwa wa wilaya hiyo.
Shimo hili linalotajwa kuwa moja ya vivutio mkoani
Mtwara limesheheni hifadhi za misitu, mito, mabonde, mawe ambayo
yanapendeza kwa macho pia kipo kisima cha maji Newala.
Jambo hili linawasumbua wale wanaojua historia
yake ni taarifa za kutupwa kwa watoto, kupotea kwa watu wale wanaojaribu
kuingia bila ruhusu, wabishi wasioamini tambiko na mambo mengine kadhaa
ambayo hata hivyo ni vigumu kuyathibitisha.
Ni shimo la asili ambalo limekuwapo miaka mingi,
na wenyeji wa Mji wa Newala wanaliita ‘Shimo la Mungu’ kutokana na kile
wanachoeleza kuwa ni maajabu ambayo hutokea yakianzia katika shimo hilo.
Miongoni mwa maajabu hayo ni yale ambayo hutokea
nyakati za asubuhi kipindi cha masika ambapo upepo mkali sana huvuma
kutoka lilipo shimo hilo.
Wanasema wakati mwingine hutokea moshi mzito ambao
husambaa na kuufunika Mji wa Newala na kusababisha giza nene katika
makazi ya watu kiasi cha watu kushindwa kuonana kwa kati ya dakika tatu
na dakika saba.
Mkazi wa Newala, Sophia Saidi (90) anasema: “Sisi
tumezaliwa tumelikuta, kutokana na shimo hilo kutotengenezwa na mtu
yeyote ndio maana tukaliita ‘Shimo la Mungu”.
Bibi Sophia kama anavyojulikana na wengine anasema
anaongeza: “Sehemu hiyo huwa panatokea miujiza kama hiyo ambayo inaleta
upepo mkali, mara giza hata sisi hatujuwi ni nani ambaye ana sababisha
kuwe na giza kutoka sehemu ya shimo hilo hadi sehemu ya makazi ya watu”.
Kutokana na umaarufu wake, eneo hilo limekuwa
kivutio kikubwa cha watu ambao hufika kwa ajili ya kufanya matambiko ya
jadi, ikiwa ni sehemu ya mila na desturi za wakazi wa Newala na wilaya
nyingine jirani.
Maimuna Pinda (55) ambaye pia ni mwenyeji wa eneo
hilo anasema hata waganga wa jadi kuingia na kutoka ndani ya ‘Shimo la
Mungu’ kwa ajili ya kuchukua dawa mbalimbali za miti shamba ambazo
hutumika kutibia magonjwa kadhaa. Pinda anasema kabla ya mtu hajaingia
ndani ya shimo hilo ili kutalii au kuchukua dawa, lazima afanywe
tambiko.
Pembezoni mwa shimo hilo huota uyoga ambao ni
kitoweo kwa wakazi wanaolizunguka, lakini kwa maelezo ya wenyeji
uchumaji huo huwa ni hatari kwani mara kadhaa watu wamepoteza maisha
kutokana na kupatwa na kizunguzungu kisha kutumbukia kwenye shimo.
Ndege hazipiti