BUNGE LA KATIBA KUANZA LEO

Tanzanian Bunge (Parliament) in Dodoma
HISTORIA ya nchi imeandikwa leo kwa Bunge Maalumu la Katiba kuanza mkutano wake huku mchakato wa kupata Mwenyekiti wa Bunge hilo, ukiwa umetangazwa kutoa nafasi kwa wajumbe wenye sifa kuingia kwenye kinyang’anyiro.
Kiongozi huyo wa Bunge na Makamu wake, wanatarajiwa kupatikana Ijumaa baada ya Kanuni za Bunge Maalumu kuandaliwa na kupitishwa leo.
Katika kikao cha kwanza cha Bunge Maalumu, mjini hapa, atachaguliwa Mwenyekiti wa muda mwenye jukumu la kusimamia na kuongoza Bunge katika kusimamia uandaaji na upitishwaji wa Kanuni za Bunge na pia kuendesha uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu.
“Tumetoa tangazo kama notisi, ili mjumbe yeyote ambaye anaona ana sifa za kazi za kuandaa kanuni na kusimamia uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu wake, ajaze fomu,” alisema Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah jana alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kwamba fomu hizo zimeshatolewa.
Kutokana na kutokuwepo Kanuni, Mwenyekiti wa muda wala Mwenyekiti wa kudumu, kikao cha kawaida cha leo asubuhi, kinaongozwa na Katibu wa Bunge, Kashililah pamoja na Katibu wa Baraza, Yahya Khamis Hamad, kwa kuelekeza wabunge namna ya kukaa na jiografia ya ukumbi.
Katika kikao cha saa 8 mchana, makatibu hao wataingia bungeni wakiongozwa na askari na kukalia kiti cha makatibu.
Lakini utaratibu waliouandaa ni kwamba watachagua mmoja wa wajumbe kukalia kiti kuongoza kazi ya uchaguzi wa mwenyekiti wa muda. Akizungumzia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Dk Kashililah alisema uchaguzi utaainishwa kulingana na kanuni zitakazopitishwa.
“Uchaguzi (Mwenyekiti) utafanywa kwa mujibu wa kanuni,” alisisitiza Dk Kashililah.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu anapaswa kuwa na taaluma ya Sheria na mwenye uzoefu wa kuongoza mikutano.
Vile vile asiwe mtu aliyewahi kuhukumiwa na kufungwa kifungo jela kinachozidi miezi sita kwa makosa yoyote yanayohusu ukosefu wa uaminifu.
Wakati huo huo, licha ya uchaguzi sanjari na kupitishwa kwa kanuni, ratiba inaonesha pia litasomwa tangazo la kuitishwa bunge maalumu. Kesho na keshokutwa kutakuwa na kikao cha kazi ya kuandaa rasimu ya kanuni za bunge.
Ijumaa wabunge watapitisha azimio la kuridhia kanuni, uchaguzi wa mwenyekiti na pia Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu wataapishwa.
Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti wa Bunge pamoja na wajumbe wataapishwa Jumamosi na kesho yake, shughuli ya kuapisha wajumbe itaendelea kabla ya ufunguzi rasmi kufanyika Jumatatu ijayo.

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family