WENGI wamesikia
historia ya wale mapacha walioungana kiwiliwili; baada ya kimya chao cha muda
mrefu wengi watapenda kujua wako wapi na wanafanya nini?
Wanafunzi hao
Maria Mwakikuti na Consolata Mwakikuti wanasoma shule ya sekondari ya Nyota ya
Asubuhi iliyopo Kidabaga, wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Uongozi wa shule
umeweka masharti magumu kidogo ili kukutana nao, lakini mtandao huu unaendelea
kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo ili watanzania waweze kujua maendeleo yao.
Kwa wasiofahamu mapacha
hao, ni wenyeji wa wilaya ya Makete mkoani Njombe; wilayani humo wanaishi
katika kijiji cha Ikonda, hapo ndipo walipozaliwa na kumalizia elimu yao ya
msingi.
Walipokuwa wakimaliza
elimu ya msingi, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja
walisema wanataka kuwa wataalamu wa kompyuta.
Miaka mitatu
sasa imepita toka wawakilishi wa mtandao huu wakutane nao katika hafla ya
kuwapongeza baada ya kufaulu vizuri mitihani yao ya darasa la saba.
Wapo kidato cha
nne katika shule hiyo ya Nyota ya Asubuhi; walijiunga na shule hiyo baada ya
walezi wao kukataa wasijiunge na shule ya sekondari ya Jangwani walikokuwa
wamepangiwa baada ya matokeo yao kutoka
Hivi sasa wana miaka 17. wanaukaribia utu uzima, kwa vyovyote watakuwa
na mengi ya kuzungumza kuhusu maisha yao ya sasa, elimu yao, changamoto
wanazopata na matarajio yao ya baadaye.