Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ameelezea kushangazwa na mauaji yanayotokea mara kwa mara nchini, akisema kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kutoa roho ya mtu. (HM)
Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika
Usharika wa Kimashuku wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
wakati wa harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi
wa kanisa hilo.
"Mtu anarudi nyumbani na anapofika
getini anauawa wakati hakuna mahali katika vitabu vitakatifu kuna
maelekezo ya baadhi ya watu kuwa na haki ya kutoa roho za wenzao,"
alisema Sumaye.
Katika harambee hiyo ambayo
ilihudhuriwa pia na Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Dk
Erasto Kweka na viongozi mbalimbali wa dini na kisiasa, Sumaye
alichangia Sh1 milioni.
Akizungumzia suala la rushwa, alisema
hivi sasa Tanzania inaongoza kwa rushwa eneo la Afrika Mashariki na kama
hatua za haraka hazitachukuliwa kuidhibiti nchi itaikaribia Nigeria.
Kanisa hilo lililopo Mailisita
wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, linahitaji Sh400 milioni kwa ajili ya
kukamilisha kazi ya ujenzi.
Sumaye alisema kuongezeka kwa matukio
ya mauaji kwa watu wasio na hatia ni matokeo ya kumomonyoka kwa maadili.
Sumaye alisema ni jambo linalotaka kuzoeleka nchini kwamba, mwananchi
anapohitaji huduma ni lazima adaiwe rushwa ili kupata huduma huku
wengine wakinyanyaswa kijinsia. Chanzo: Mwananchi