Mh Edward Lowassa |
ALIYEKUWA Waziri Mkuu na Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa (CCM), ameitaka Serikali kuainisha vipaumbele
vichache katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2014/2015 na
kushauri kipaumbele kikuu kiwe ajira kwa vijana.
Aidha, amesema serikali ni lazima ifanye
uamuzi mgumu katika kushughulikia changamoto zinazoikabili, badala ya
viongozi na wananchi kulalamika kila wakati.
Lowassa aliyekuwa akichangia mjadala wa
mapendekezo ya mpango huo bungeni jana, alisema kuwa kamwe mipango ya
Taifa haiwezi kutekelezeka, ikiwa serikali haitatenga vipaumbele
vichache na muhimu, tofauti na ilivyo sasa kwamba mpango umekuja na
vipaumbele vingi.
Katika mpango huo, serikali imeainisha
vipaumbele sita ambavyo ni; miundombinu; kilimo; viwanda vinavyotumia
malighafi za ndani na kuongeza thamani; rasilimali watu na ujuzi;
uendelezaji huduma za utalii na biashara na fedha. Lowassa alisema
angekuwa yeye kiongozi, angeanza na kipaumbele cha ajira, elimu, Reli ya
Kati, foleni Dar es Salaam na katika suala la Afrika Mashariki,
angeweka nguvu ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Alisema hakuna mpango wowote wa maendeleo katika taifa lolote, unaweza kufanikiwa ikiwa kuna tatizo la ajira, hasa kwa vijana.
Alikumbusha kuwa mitaani kuna vijana
wengi, waliomaliza vyuo vikuu, kidato cha nne, sita na darasa la saba,
hawana ajira na ikiwa Serikali haitachukua uamuzi mgumu kushughulikia
suala hilo, litaigharimu baadae.
“Tusipowashughulikia, watakula sahani
moja na sisi, tusipoangalia yatatufika yale ya wenzetu wa Afrika
Kaskazini, tuangalie suala ajira kwa umakini sana, ajira kwa vijana
inawezekana sana kila mmoja akitekeleza wajibu wake,” alisema Lowassa.
Alitoa mfano kwa nchi ya Hispania iliyokuwa na tatizo kubwa la ajira
mara baada ya kutokea kwa mdororo wa uchumi dunia, Lowassa alisema baada
ya tatizo hilo, nchi hiyo ilikaa na kuamua kulitafutia ufumbuzi kwa
kuweka masharti kwa kila mwekezaji anayeingia kuwekeza nchini humo, atoe
ajira kwa vijana.
Alisema Hispania iliyokuwa na tatizo
hilo kwa zaidi ya asilimia 50, baada ya miaka miwili walipiga hatua na
sasa tatizo hilo limeondoka.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Fatuma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kwa kuamua
kuangalia suala la ajira kwa vijana na kuwapa matrekta na mashamba kwa
ajili ya kilimo cha vitunguu.
Kuhusu elimu, alisema ipo haja ya kuwa
na mjadala wa elimu wa taifa na kelele zinazopigwa na wananchi kuhusu
elimu, zisipuuzwe kwa kuwa lipo tatizo la msingi katika sekta hiyo hapa
nchini.
Alisema kulikuwa na haja ya tume
iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza matatizo ya elimu hapa nchini,
kutoa taarifa bungeni ijadiliwe ili wabunge wajue matatizo yaliyopo na
namna ya kuyatatua.
“Haitoshi kuchukua wanafunzi wengi
kumaliza chuo kikuu wakati akiingia sokoni digrii anayoipata, anakosa
kazi anayotakiwa kuifanya, wenzetu Ujerumani wanagawa wenye digrii nusu
na hawa wenye ujuzi nusu, mwenye ujuzi na digrii ana uhakika wa ajira,
hapa hawana uhakika wa ajira kwa sababu ya aina ya elimu tunayotoa,”
alisema Lowassa.
Lowassa alisema nchi isipokuwa makini
kushughulikia suala la elimu, itaachwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumzia suala la barabara, Lowassa
alimpongeza Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kwa hatua kubwa ya ujenzi
barabara nchini na alishauri pamoja na hatua hiyo ya Serikali kujenga
barabara kwa kiwango cha lami, nyingi zinaharibika kwa kasi ya hali ya
juu, kutokana na uzito wa mizigo inayopaswa kusafirishwa kwa reli,
kusafirishwa kwa malori.
Aidha, alisema foleni katika Jiji la Dar
es Salaam ni kero kubwa, inayochangia kuyumbisha uchumi wa nchi,
kutokana na watu wengi kutumia muda mrefu barabarani wanapokwenda
kazini, hivyo kushauri suluhisho la kudumu, liwe sasa na si kusubiri
zaidi.
Hata hivyo, alimpongeza Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwa kazi nzuri, anayofanya kutatua kero
hiyo jijini humo na kushauri kuongeza juhudi ya suluhu ya tatizo hilo.
Lowassa aliipongeza Serikali kuanzisha
Chombo cha Kusimamia Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Programu na Miradi ya
Maendeleo chini ya Ofisi ya Rais (PDB) na kutaka kipewe meno ili kuleta
mafanikio katika mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa.
“Tatizo la nchi yetu, tunazungumza mambo
hakuna utekelezaji, Malaysia kuna nidhamu lakini hapa kwetu uswahili
mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, kinatakiwa chombo kinachoweza
kuchukua na kufanya uamuzi mgumu, haiwezekani nchi ikawa ya kulalamika
tu, kiongozi analalamika, mwananchi analalamika, hatuwezi kuwa jamii ya
kulalamika, lazima awepo wa kuchukua hatua na kufanya uamuzi,”
alisisitiza Lowassa.
Kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Lowassa alishauri kutogombana na viongozi wa jumuiya hiyo akiwemo Rais
Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museven wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa
Kenya kwa uamuzi wao wa kwenda Sudan Kusini badala yake Tanzania iende
Mashariki mwa Kongo, ambako ni kuzuri zaidi.
Pia alishauri Reli ya Kati iimarishwe na kufufuliwa kuwa chanzo kikuu cha uchumi.