POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inashikilia watu sita kwa
tuhuma za kuvamia, kupora na kumjeruhi kwa mapanga Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa
watuhumiwa hao walikamatwa katika msako, uliofanywa na Polisi maeneo ya
Mpiji Magohe mpakani mwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, baada ya
uvamizi huo uliofanyika juzi usiku.
Alisema mara baada ya tukio hilo, polisi walianzisha msako kuanzia
eneo hilo kwa ushirikiano na raia wema na watuhumiwa hao walitiliwa
shaka na kukamatwa.
Kwa sasa majina yao yamehifadhiwa kwa sababu upelelezi bado
unaendelea. Kwa mujibu wa Kamanda Kova, baada ya watuhumiwa hao
kupekuliwa, walikutwa na bangi puli 17 na pombe haramu ya gongo lita 15.
Kova alisema msako unaendelea kwa kushirikiana na Polisi mkoa wa
Pwani, ili kuhakikisha aliyehusika na uvamizi huo anakamatwa ili
kukamilisha hatua za kiupelelezi na hatimaye kufikishwa mahakamani.
Alisema anaamini bado wapo watuhumiwa zaidi, waliohusika na tukio
hilo na Polisi itahakikisha wote wanapatikana. Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema watu sita wanaodhaniwa kuwa
majambazi, walivamia nyumba ya Dk Mvungi saa saba usiku na kumlazimisha
awape fedha.
Alisema wakati wa mabishano, walimcharanga na mapanga na kufanikiwa kukimbia na baadhi ya vifaa na fedha.
“Alijeruhiwa mwilini hasa kichwani na baada ya uvamizi huo,
alikimbizwa katika hospitali ya Tumbi, Pwani ambako alipatiwa huduma ya
kwanza na kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi,” alisema.
Afya yaimarika
Ofisa Uhusiano wa Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MOI), Jumaa Almasi, alisema hali ya mwanasiasa huyo inaanza
kuimarika na ameanza kuzungumza taratibu.
Dk Mvungi ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo,
pia ni Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa Chama cha NCCR- Mageuzi.
Hata hivyo, waandishi wa habari na wapigapicha walizuiwa kuingia
kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU),
alimolazwa Dk Mvungi.
“Tungeweza kuruhusu muingie na kuzungumza naye kuhusu yaliyompata,
lakini kwa kweli hali yake si nzuri na hatakiwi kuzungumza,” alisisitiza
Almasi.
JK, Bilal wamjulia hali
Juzi Rais Jakaya Kikwete alimtembelea na kumjulia hali Dk Mvungi,
akifuatana na Mama Salma Kikwete, ambapo alijionea mwenyewe hali yake.
Jana Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal naye alipata fursa kama
hiyo na kuweza kumwona majeruhi huyo. Pia, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na mjumbe wa Tume hiyo, Dk
Salim Ahmed Salim walifika hospitalini hapo kumtembelea na kumjulia hali
mwenzao.
Viongozi wote hao wa juu kitaifa waliambiwa kwa nyakati tofauti,
kwamba watu hao wanaodhaniwa kuwa kati ya wanne na saba, waliiba simu
mbili za mkononi, laptop, fedha taslimu zinazokadiriwa kufikia Sh
milioni moja na bastola ya Dk Mvungi.
Imeandikwa na Halima Mlacha na Hellen Mlacky.