WATANGAZAJI WAKIMZUNGUMZIA MAREHEMU JULIUS NYAISANGA KWA MASIKITIKO

Julius Nyaisangah enzi za uhai wake.
Makala: Brighton Masalu
KILA nafsi itaonja mauti. Aliyekuwa mtangazaji wa kimataifa, Julius Nyaisangah ametangulia mbele za haki. Hapa ni baadhi ya watangazaji waliowahi kufanya kazi na wakijaribu kueleza hisia zao.
ABDALLAH MUSA MWAIPAYA:“Nilikutana na Nyaisangah pale Mwenge kuna baa moja iitwayo Maryland nikiwa na mwenzangu Ezekiel Malongo. Tangu siku hiyo tukawa marafiki kwani alikuwa akinivutia sana katika kazi za utangazaji, alikuwa na sauti ya kuvutia kwa kusoma taarifa ya habari sijawahi kuona.”



ISAAC MUYENJWA GAMBA:
“Nilikutana kwa mara ya kwanza na Nyaisangah kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza 1997 alipoenda Mwanza akiwa na bendi ya muziki ya Dar es Salaam Kibindankoi akiwa kama afisa uhusiano wa bendi hiyo.
Alikuwa mwalimu mzuri wa utangazaji kwangu, mshumaa umezimika.”

ABUBAKAR SADICK ‘Kwa Fujo’
“Nilikutana na Nyaisangah mwaka 1999 pale Radio One akiwa mkurugenzi msaidizi. Hakika sitamsahau Nyaisangah. Alikuwa kama babu yangu katika kazi za habari”.

BETTY MKWASSA:
Huyu kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani  Dodoma, aliwahi kufanya kazi na marehemu Nyaisangah. “Alinipokea pale Redio Tanzani Dar es Salaam akiwa na Ahmed Kipozi. Hata Radio One na ITV alinipokea yeye pamoja na Charles Hillary.  Sikuwahi kumuona akiwa amechukia. Hakika alikuwa mcheshi, alijua vyema kukitumia Kiswahili na haikuwa rahisi kugundua alitoka mkoa gani.”
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family