KAMANDA MSTAAFU WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI NCHINI AFARIKI DUNIA

SACP mstaafu James Kombe enzi za uhai wake.
Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (Mstaafu) James Kombe amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kifo hicho Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema, Kombe alifariki Oktoba 22 mwaka huu na taratibu za mazishi  zinaendelea nyumbani kwa mtoto wake, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.
Aidha habari tulizozipata kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema marehemu atasafirishwa na kupelekwa Moshi kwa mazishi kesho Oktoba 23.
Akizungumzia historia yake, Kamanda Senso alisema marehemu Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na jeshi la polisi Machi 15, 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda.
Akiwa mtumishi wa jeshi hilo Kombe alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni pamoja na Sagenti wa Polisi (1973), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi(1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.
Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia katika Jeshi la Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha, Kigoma pamoja na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Tanzania (FFU) na hadi anastaafu alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family