BAADHI ya wananchi wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Vipimo
(WMA) kwa kuanzisha kanuni ya kusimamia biashara ya gesi ya kupikia
iliyofungashwa kwenye mitungi na inatotumika sana nyumbani na hotelini
(LPG) na kusema kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha maisha yao na
hatimaye kupunguza uharibifu wa mazingira.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wanasema kabla ya
kanuni hiyo kutungwa ilikuwa ni vigumu sana kwao kufahamu haki zao
wanapokwenda kununua gesi hiyo ya mitungi, kwani kanuni haikuwa wazi
kuhusu biashara hiyo.
Rehema Tendwa wa Dar es Salaam anasema iwapo kanuni hiyo itatekelezwa
ipasavyo itachochea ukuaji wa biashara hiyo kutokana na wananchi kuwa
na imani na huduma wanayoipata kutokana na ujazo wa gesi kwenye mitungi
kulingana na thamani ya pesa yao na hivyo matumizi ya nishati ya mkaa na
kuni kupungua na hivyo kusaidia kutunza mazingira yetu.
Shabu Kibaja wa Temeke ambaye amekuwa akitumia gesi kwa muda mrefu
kupikia, anaona kuwa kanuni hiyo itatekelezwa kikamilifu, ni dhahiri
wateja wa mitungi hiyo wataweza kupata haki yao.
Rashid Bwela wa Kibaha mkoani Pwani anasema: “Kuna makampuni mengine
yanayouza gesi yanaweka gesi kidogo kwenye mitungi yao wakati kuna
mengine angalau yanaweka ya kutosha, yaani biashara hii ni holela, na
hakika kwamba kanuni hiyo itatusaidia kuwa na huduma moja inayoeleweka.”
Beatus Kapama, mkazi wa Ukonga Jijini Dar es Salaam, anaipongeza
serikali kuwa kuchukua hatua hiyo katika kipindi hiki. Anasema biashara
hiyo imeshamiri kutokana na maendeleo ya kiuchumi yanayotokea hapa
nchini kwa sasa na pia itasaidia katika kupunguza uharibifu wa
mazingira.
“Kwa kweli kanuni hii imekuja wakati muafaka, wananchi wengi
wanatumia gesi tofauti na hapo awali ambako walikuwa wanatumia mkaa na
kuni, hivyo kuchangia uharibifu wa mazingira kwa kweli kuna maendeleo,
hivyo uwepo wa kanuni inayosimamia biashara hiyo ni jambo jema sana
kwani pia biashara hiyo itakua zaidi,”anasema.
Mwajuma Ally, Mkazi wa Unguja, Zanzibar, anaipongeza serikali kwa
kuanzisha kanuni hiyo na kwamba inalenga katika kumkomboa mnyonge,
hususan mwanamke ambaye ndiye husumbuka sana na kuni. “Ni kanuni muafaka
kwa kweli inatulenga sisi watu wa hali ya kawaida, hususan mwanamke na
iwapo itatumika vizuri ni dhahiri kwamba haki zetu kama watumiaji wa
gesi majumbani zitalindwa,” anasema.
Mwajuma ambaye anasema kupikia gesi kuna raha kulinganisha kuni na
mkaa, anaomba uwepo utekelezaji wa makini wa kanuni hiyo ili kuhakikisha
kwamba malengo ya utungwaji wa kanuni hiyo yanatekelezwa. John Masanja
mkazi wa Mwanza naye anasema kwamba serikali imeleta kanuni muafaka na
kwa muda muafaka.
Akiongea kwa simu, Masanja anasema: “Hizi biashara za gesi zinazidi
kukua kila kukicha naona serikali imekuja na kanuni muafaka kabisa.
Naipongeza na ninaomba wote tushirikiane katika kuitekeleza”. Simon
Mwakasege, Mwanasheria wa Jijini Dar es Salaam anaipongeza serikali kwa
kuanzisha kanuni hiyo na kusema kwamba itasaidia kudhibiti biashara
holela ya gesi hapa nchini.
“Nadhani kanuni hii italeta usawa katika biashara hii ya gesi hapa
nchini. Wakati kulipokuwa hakuna kanuni wananchi walikuwa hawajui
usahihi kabisa wa vipimo katika biashara hii, walikuwa na imani tu
kwamba kampuni hii wanajaza gesi vizuri, wale wanapunja, basi, ilimradi
tu ilikuwa ni vurugu, hivyo ni matumaini yangu kwamba kanuni hii
itasaidia kuleta usawa katika biashara hii,” anasema.
Anasema kutokana na kukua kwa matumizi ya bidhaa za gesi hapa nchini
ni dhahiri kwamba kanuni maalumu ni lazima iwepo ili kuwalinda watumiaji
na hata wauzaji. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Tanzania inapoteza
kiasi cha hekta 400,000 za misitu kila mwaka kwa sababu ya ukataji miti
unaochochewa na matumizi ya kuni, mkaa, mbao, ujenzi ama uchomaji moto
misitu.
Akizungumza hivi karibuni Mkoani Rukwa katika maadhimisho ya Siku ya
Mazingira duniani, Pinda alisema utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi
wake wa Tathmini ya Rasilimali za Misitu unaonesha kuwa ukataji huo wa
misitu unasababisha kuzalishwa kwa tani milioni moja za mkaa ambao nusu
yake unatumiwa na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
“Tanzania inakadiriwa kuzalisha kiasi cha tani milioni moja za mkaa
kila mwaka, nusu yake, yaani tani 500,000 zinatumika Dar es Salaam peke
yake. Kuni zinatumika sana vijijini wakati mkaa unatumika sana mijini.
Ndiyo sababu tunasisitiza kwamba, kama tukiwapatia wakazi wa mijini
hususan wale wa Dar es Salaam nishati mbadala kama vile gesi, umeme na
nishati itokanayo na jua, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa ukataji
miti nchini kwa ajili ya kutengeneza mkaa,” anasema.
Baadhi ya wabunge wameitaka serikali kuhimiza matumizi ya nishati
mbadala, ili kupunguza athari za mazingira zitokanazo na matumizi ya
kuni na mkaa kwenye maeneo ya mijini na vijijini. Wabunge hao Diana
Chilolo, Magdalena Sakaya (viti Maalum) Juma Kilimba (Iramba Magharibi),
wanasisitiza umuhimu wa nishati mbadala kama vile gesi ya kupikia
majumbani.
Wabunge hao wanasema kwa kiasi kikubwa mazingira yamekuwa
yakiharibiwa kutokana na ukataji miti kwa wingi kwa matumizi ya nishati
na hivyo kusababisha ukame. Wanaishauri serikali kuhimiza matumizi
mbadala ya nishati kwa matumizi ya majumbani ili kukabiliana na
uharibifu mkubwa wa mazingira.
Hivi karibuni serikali kupitia WMA, imepitisha kanuni ya kusimamia
biashara ya gesi ya majumbani na hotelini ili kukabiliana na upungufu
yaliyojitokeza katika uendeshaji wa biashara hiyo hapa nchini. Wakala wa
Vipimo (WMA) ulioko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, jukumu lake
kubwa ikiwa ni kumlinda mlaji kupitia usimamizi wa matumizi sahihi ya
vipimo katika biashara, afya, usalama na mazingira.
Kazi kubwa ya WMA ni kuhakikisha kwamba vipimo vya bidhaa zinazouzwa
kwa mteja zinalingana na thamani ya pesa yake. Mbali na kupitisha kanuni
hiyo, serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa nishati mbadala kama vile
gesi ya kupikia majumbani ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira
unaosababishwa na matumizi makubwa nishati ya mkaa na kuni.
Magdalena Chuwa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo yenye Makao
yake Makuu katika jengo la Mwalimu lililopo mtaa wa Uhuru, Ilala, jijini
Dar Salaam.
Anasema pamoja na jukumu la uhakiki wa vipimo vya bidhaa mbalimbali
ambao unafanywa na wakala wake, kwa miezi kadhaa iliyopita wakala
ulielekeza nguvu zake katika kuandaa kanuni watakayotumia kusimamia
vipimo vya matumizi ya gesi ya kupikia na anasema ni jambo la faraja
kuona kwamba kanuni hiyo sasa inaanza kutumika rasmi.
Awali ya yote anatoa shukrani kwa wadau mbalimbali walioshiriki
katika zoezi hilo muhimu na kwamba mawazo yao yalisaidia sana katika
kufanikisha upatikanaji wa kanuni hiyo. “Lengo la kuiandaa kanuni hiyo
ni kuhakikisha kwamba watumiaji wa gesi ya kupikia, wasambazaji na wadau
wengine wote wanatumia vipimo sahihi kwa mujibu wa sheria za nchi ili
Tanzania iweze kunufaika na rasilimali hii muhimu katika uchumi wake,”
anasema.
Chuwa anasema hatimaye Kanuni hiyo imekamilika na tayari imeanza
kutumika. Anasema kwamba kanuni hii imekamilika baada ya kuwashirikisha
wadau mbalimbali ambao kwa kupitia vikao kadhaa walitoa maoni yao na
baadaye kufanyiwa kazi ipasavyo na Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Wakala wa Vipimo (WMA) ambao kazi yao ni pamoja na kusimamia matumizi
sahihi ya vipimo katika biashara, walikuwa wakiandaa kanuni
itakayosaidia kusimamia uuzaji wa gesi hiyo inayotumika majumbani kwa
ajili ya kupikia.
Chuwa anafafanua kuwa Kanuni hiyo imesainiwa na Waziri wa Viwanda na
Biashara, Dk Abdallah Kigoda na tayari inatumika baada ya kutangazwa
katika gazeti la serikali (GN) No. 222 la tarehe 19/07/2013 Anasema LPG
ni aina ya gesi inayotokana na bidhaa za petroli ambayo huagizwa kutoka
nje ya nchi kupitia makampuni yanayoagiza mafuta au bidhaa za petroli.
“Husafirishwa kwa meli na kupakuliwa kupitia mabomba maalumu na
hatimaye kuhifadhiwa katika matangi makubwa kabla ya kupakiwa/kujazwa
kwenye mitungi midogo midogo yenye uzito tofauti tofauti tayari
kusambazwa kwa watumiaji. Chuwa anazidi kusema: “Ni ukweli usiopingika
kuwa, hivi sasa nishati ya gesi imechukuwa nafasi kubwa sana katika
jamii kwa matumizi ya kupikia majumbani kutokana na nishati nyingine
kama kuni, mafuta ya taa na hata umeme kuwa na gharama za juu sana au
upatikanaji wake kutokuwa wa uhakika.
Kutokana na hali hiyo, gesi imekuwa biashara kubwa nchini na hivyo
kusababisha makampuni mengi hasa yale yanayosambaza nishati ya mafuta
kujiingiza pia katika biashara ya gesi ya kupikia ili kukidhi mahitaji
ya soko.
“Ni matarajio ya Serikali kuwa biashara ya gesi hususani ya majumbani
itafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Vipimo pamoja na Kanuni zake, hasa
katika eneo la vipimo vya uzito wa mitungi ya gesi ili kuhakikisha
kwamba msambazaji na mtumiaji kila mmoja anapata haki yake kulingana na
thamani ya pesa yake.”
Chuwa anafafanua kuwa uchunguzi uliowahi kufanywa na Wakala wa Vipimo
ulikuwa umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara hasa mawakala walikuwa
wanatumia ujanja katika kujiongezea faida kwa kupunguza uzito wa mitungi
ya gesi na kupakia katika mitungi midogo midogo.
Aidha, uchunguzi huo ulibaini pia mapungufu mengi ya kiufundi, mfano
ulikuwa ukiangalia mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) ilivyoandikwa utaona
kuwa kila kampuni inayosambaza gesi kwa matumizi ya majumbani imekuwa
ikiandika taarifa katika mitungi yao kwa jinsi wanavyojua wao na hivyo
kuwachanganya wateja jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Moses Mbunda ni Mwanasheria wa Wakala wa Vipimo. Yeye anafafanua kuwa
kuhusu madhumuni ya kanuni hiyo kuwa ni kuhakikisha kuwa biashara ya
gesi hapa nchini inafanyika kwa haki na hivyo kuwalinda watumiaji.
“Kanuni hiyo mpya inataka makampuni na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo
kuzingatia kuwa, vipimo vyote vitakavyotumika ni vile vinavyotumia
mfumo wa kimataifa (SI units) ambavyo nchi yetu imeridhia,” anasema.
Anaongeza kuwa mfumo huu wa vipimo utumike hususani katika kuelezea
uzito wa mtungi ulio tupu (tare weight), uzito wa gesi peke yake (net
weight) na ule uzito wa mtungi na gesi (gross weight).
Mbunda anasema kanuni hiyo inabainisha kuwa mtungi uliobeba gesi ni
sharti uwe na maandishi yanayoonesha utambulisho wa bidhaa hiyo, jina la
kampuni inayosambaza, namba ya mtungi, uzito wa mtungi bila gesi, uzito
wa gesi peke yake na uzito wa mtungi pamoja na gesi.
Kanuni hiyo pia inawataka wafanyabiashara wa gesi iliyofungashwa
kwenye mitungi kuwa na mizani katika kila eneo la biashara kwa ajili ya
kuhakikisha uzito wa bidhaa hiyo pindi mteja anapokuwa amenunua.
Wakaguzi kutoka Wakala wa Vipimo watapita kila eneo la biashara
kukagua kama mfanyabiashara huyo anayo mizani iliyothibitishwa na Wakala
wa Vipimo na kwamba kanuni zote zinazotakiwa kuwa zimezingatiwa katika
ufungashaji wa bidhaa hiyo. Mbunda anasema Wakala wa Vipimo utasimamia
ipasavyo, utekelezaji wa kanuni hiyo mpya kwa lengo la kuwalinda
watumiaji.