BAADA ya kukaa bila waume na wake kwa
zaidi ya mwezi mmoja sasa kutokana Operesheni Kimbunga, Serikali
imetangaza kuwa itatoa fomu maalumu ili kuwarejesha nchini wahamiaji
haramu walioolewa au kuoa nchini ili waungane na familia zao.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta aliyasema hayo mjini hapa alipokuwa akizungumza
na waumini wa Kanisa Katoliki waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kanda
ya Mungu ni Mwema ya Kwaya ya Kapotive ya mjini Bukoba. Waziri Sitta
alisema;
“Serikali imeamua sasa kwamba watarudi
nchini lakini watajaza fomu maalumu za kuwawezesha kuishi ili waungane
na familia zao na kuendelea kufurahia maisha ya ndoa na familia.
“Tumeona tufanye hivyo kwani si kazi ya
serikali kuvunja ndoa za watu. Lakini katika kuchukua hatua hiyo
tutakuwa makini kuhakikisha kuwa wahamiaji wahalifu hawarejei nchini,”
alisema. Alisema,
“Nawahakikishia kuwa enzi wa wahalifu
sasa basi. Rais (Jakaya Kikwete) hakutangaza operesheni hii hivi hivi,
bali alichoshwa na matukio ya uhalifu yaliyokuwa yanatokea.
“Enzi za wananchi wetu kushushwa kwenye
mabasi na kuporwa, misitu yetu kuvamiwa na wahamiaji hawa wakiwa na
idadi kubwa ya mifugo na pia vijiji vyetu kuvamiwa na wageni na kutumia
fedha zao, kufundisha kwa mitaala yao na kupeperusha bendera za nchi zao
ndani ya Tanzania sasa basi,” alisema Sitta.
Kauli ya Sitta inakuja baada ya kuwepo
kwa malalamiko hasa katika maeneo ya mipakani kwa operesheni kimbunga,
kusababisha ndoa nyingi kuvunjika, kutokana na wanaume au wanawake
waliooa au kuolewa nchini kukumbwa na operesheni kimbunga na kuziacha
familia zikiteseka.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constatine
Kanyasu alimwambia Sitta alipotembelea mpaka wa Rusumo hivi karibuni,
kwamba wanaume wengi wa Tanzania wanaoa Rwanda kutokana na mahari kuwa
ndogo kuliko wakioa Watanzania na pia kutokana na Wanyarwanda kuwa na
sura na maumbo ya kuvutia.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema
pamoja na kufurahishwa na hayo lakini wanandoa hao wamekuwa wakishindwa
kulipa ada ya Dola za Marekani 550, zinazotozwa kila baada ya miaka
miwili ili kuwawezesha wenzi wao kuishi kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia uzinduzi wa kanda hiyo,
Sitta aliwaasa wanakwaya nchini kutumia nyimbo kuonya juu ya kuporomoka
kwa maadili nchini akisema vijana wanateketea kwa kubebeshwa dawa za
kulevya na watu wenye fedha na madaraka.
“Maadili yameshuka sana ndani ya nchi
yetu, vijana wetu sasa wamegeuzwa kuwa punda wa kubeba dawa za kulevya.
Hadi sasa vijana zaidi ya 600 wamefungwa Brazil, Singapore, Malaysia,
China, Marekani na Afrika Kusini huku baadhi wakisubiri kunyongwa,
wanakwaya tumieni nafasi hii kuomba Mungu atuepushe na janga hili,”
alisema Waziri Sitta.
Alisema janga hilo linachangiwa kwa
kiasi kikubwa na kutafuta utajiri wa haraka huku akiongeza kwa kusema;
“Sisi wazee ndio tunaopaswa kulaumiwa kwa kuwaingiza vijana katika
kutafuta utajiri wa dhambi kwa kutokuwa na roho ya huruma na kuifanya
nchi kupoteza taswira nzuri katika anga za kimataifa,” alisema.