SERIKALI imewaruhusu wamiliki wa malori
kugoma kufanya biashara yao, kama hawakubaliani na sheria iliyopo ya
kutoza wanaozidisha mizigo, ila wahakikishe wanagomea majumbani kwao na
si barabarani.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa
mgomo baridi, ulioitishwa na Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA),
uliopangwa kuanza jana kupinga tozo hiyo.
Alisema wanaotaka kuendelea na mgomo
huo, wanaweza kuendelea, lakini wahakikishe hawaleti usumbufu kwa
watumiaji wengine wa barabara.
Msemaji wa Tatoa, Elias Lukumay katika
tamko lake la kuitisha mgomo mwishoni mwa wiki, alisema kuwa mwaka 2006,
Serikali ilitoa msamaha, kwamba haitatoza magari yenye uzito usiozidi
asilimia tano, juu ya viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria baada ya
kubaini umuhimu wa msamaha huo.
Katika tamko hilo, Lukumay alisema kabla
ya kufikiwa msamaha huo, Serikali iliunda kamati iliyofanya ziara
katika mizani na kubaini zina upungufu wa kutofautiana matokeo ya
vipimo.
Mbali na upungufu wa mizani, Lukumay
alisema pia kamati hiyo ilibaini kuwa ubovu wa barabara na matuta,
umekuwa ukisababisha mizigo kuhama na kuzidisha uzito sehemu moja ya
gari.
Alifafanua kuwa kuhama kwa mizigo,
kunakosababishwa na matuta na ubovu wa barabara, husababisha ekseli, au
muunganiko mmoja wa matairi unaotumika kupima uzito, kulemewa na
kujikuta uzito ukiongezeka kutoka mizani moja kwenda nyingine, hata kama
hakuna mzigo ulioongezeka.
Kutokana na uamuzi huo wa Serikali
kwamba kuanzia Oktoba mosi mwaka huu, imefuta msamaha uliokuwa umetolewa
awali kwa magari yaliyokuwa yanapimwa na kukutwa na ongezeko lisilozidi
asilimia tano juu ya tani 56, iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria, wameamua
kuegesha magari yao popote yatakapokuwepo, ili wasiharibu barabara na
wasigombane na Dk Magufuli.
Pamoja na kauli hiyo ya Lukumay, Dk
Magufuli alisema kuwa na endapo Tatoa watatekeleza azma yao hiyo,
itakuwa nafuu kwa barabara ambazo zimekuwa zikiharibiwa, kutokana na
kuzidi uzito.
“Kama wanataka kugoma wafanye hivyo,
mbona vyuo vikuu vinakuwa na migomo na hata mtoto nyumbani ukitaka
kumlisha chakula anagoma, wanaweza kufanya hivyo kwa kuegesha magari yao
majumbani na si barabarani.
“Itakuwa vizuri sana wakigoma, maana watafanya barabara zetu zicheke,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema ni kikundi cha
wenyemalori wachache, ndio waharibifu wa barabara na kuwataka kuiga
kampuni zingine kama Bakhresa na Dar Express, ambazo alisema hata siku
moja hawazidishi uzito.
“Ninaweza kuwataja, maana wengine katika
haka kakikundi, ndio wanaongoza kwa kujaza mizigo. Sisi tunasema kuwa
tunaendelea kulinda barabara ambazo fedha za wananchi zinatumika
kujenga. Hivyo kikundi hiki hakiwezi kuendelea kupata faida kubwa
kupitia barabara,” alisema.
Juzi madereva wa malori ya mizigo
walifunga barabara ya Morogoro kwa zaidi ya saa 15, baada ya kukaidi
agizo la Serikali na kusababisha usumbufu kwa watumiaji.
“Barua ndiyo iliyowapa nafuu hiyo, na
sisi tumeirudisha kwa barua. Hakuna sheria inayovunjwa kwa barua, ila
sheria ndiyo inayoweza kufuta sheria. Sheria ipo na tutaendelea
kuisimamia. Baadhi ya kundi hilo ni wanasiasa wapeleke muswada bungeni
kubadilisha,” alisema.
"Sheria iliyopo inaruhusu mtu kuja
kukataa rufaa kwa Waziri kama ameona sheria iliyopo haifai na kama
hakuridhika na uamuzi utakaotolewa anatakiwa kwenda mahakama ya juu.
Wanaweza kwenda mahakamani tukutane huko huko,” alisema.
Magufuli alisema Tanzania ndio nchi
pekee inayoongoza kwa kuruhusu mizigo ya ukubwa wa mpaka tani 56 kuliko
nchi zinazoendelea, ambapo kwa Umoja wa Ulaya uzito ulioruhusiwa ni tani
40 hadi 45 wakati Marekani imeruhusu tani 36 tu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hali iliyojitokeza
Jumamosi, haitajitokeza tena, kwa kuwa wamejipanga kudhibiti hali hiyo.
Alionya kuwa watakaoegesha magari barabarani, watachukuliwa hatua kali
za kisheria.
“Tutahakikisha mgomo hauleti usumbufu
kwa watumiaji wengine wa barabarani na hii ndio kazi yetu,” alisema na
kuongeza kuwa mpaka sasa hajapewa taarifa ya mgomo huo, zaidi ya kusikia
na kusoma kwenye vyombo vya habari.
Gazeti hili lilitembelea barabara ya
Morogoro kuangalia kama mgomo huo umefanyika. Lakini, barabara ilikuwa
nyeupe huku mizani ya Kibaha, ikionekana kufanya kazi yake kwa mabasi na
malori kuingia na kupima mizigo yao.