Rais wa Cameroon Paul Biya amemshawishi mwanasoka Samuel Eto'o kutafakari upya mipango yake ya kujizulu kutoka soka ya kimataifa
Mshambulizi huyo wa Chelsea alikutana na
waakilishi wa Rais mjini Yaounde kujadili mustakabali wa mchezaji huyo
kuhusu soka ya kimataifa.
Baada ya kukutana na Eto'o, alikubali kuchezea Cameroon kwa mara nyingine.
Sasa atakwenda Ufaransa kujiunga na timu ya
nyumbani inayojiandaa kucheza dhidi ya Tunisia katika michuano ya kufuzu
kwa kombe la Dunia Brazil mwaka 2014.
Etoo mwenye umri wa miaka 32 aliambia wenzake
kuwa hatacheza tena soka ya nyumbani punde tu baada ya Cameroon
kuicharaza Libya na kuingia katika awamu ya pili ya kufuzu kwa kombe la
dunia.
Licha ya ripoti za yeye kuacha kucheza soka,
kocha wa timu ya Cameroon Volker Finke alimteua Eto'o kuchezea timu ya
taifa ya Cameroon dhidi ya Tunisia ingawa mwenyewe hakuwa ametoa taarifa
rasmi.
Eto'o amekuwa na uhusiano tete na maafisa wa
soka nchini Cameroon katika siku za nyuma ikiwemo hata kuongoza timu ya
taifa kwenye mgomo uliosambaratisha mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria.
Eto’o aliadhibiwa kwa kupigwa marufuku kucheza mechi 15 ingawa baada ya kukata rufaa alipunguziwa adhabu hadi mechi 8
Hata baada ya adhabu yake kumalizika alikataa kuichezea Cameroon kwa miezi kadhaa.
Pia sio mara ya kwanza kwa Rais Biya kuingilia kati na kumzuia mchezaji kujiuzulu kutoka katika majukumu ya kitaifa. |