Stori: Chande Abdallah
MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka mitatu, Maryment Ibrahim ambaye anaishi Tandale jijini Dar es Salaam, hivi karibuni alipatwa na masahibu makubwa baada ya kutekwa nyara na kutoroshwa hadi Gairo mkoani Morogoro huku mtekaji akidaiwa kutaka apewe shilingi milioni 6 ili amuachie.
MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka mitatu, Maryment Ibrahim ambaye anaishi Tandale jijini Dar es Salaam, hivi karibuni alipatwa na masahibu makubwa baada ya kutekwa nyara na kutoroshwa hadi Gairo mkoani Morogoro huku mtekaji akidaiwa kutaka apewe shilingi milioni 6 ili amuachie.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Oktoba 16 mwaka huu baada ya
kijana mmoja, anayefanya biashara ya kuuza chipsi anayejulikana kwa jina
la Issa Ramadhani, kudaiwa kumchukua mtoto huyo aliyekuwa akicheza
nyumbani kwao na kutoweka naye kabla ya wazazi wake kubaini na kwenda
kutoa taarifa kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’.
Awali, ilidaiwa Ramadhan alikuwa na tabia ya kuwachukua watoto wadogo
wa mtaani hapo na kuondoka nao na kuwarudisha baadaye, kitu
kilichowafanya wazazi wa mtoto huyo kutokuwa na wasiwasi.
Wakizungumza na mwandishi wetu, wazazi wa mtoto huyo walisema
waliamua kutoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada nambari
KJM/RB/8994/13 baada ya kupashwa kuwa mtekaji ambaye alishaacha kazi
yake ya kukaanga chipsi, aliondoka muda mrefu na binti yao na hakukuwa
na dalili za kurejea.
Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, wazazi hao pamoja na majirani
walifanya uchunguzi wa chinichini na kufanikiwa kupata namba ya simu ya
mtekaji huyo, lakini walifanikiwa kubadilishana naye ujumbe mfupi wa
simu kwani hakuwa akipokea simu yake ya kiganjani.
Inadaiwa kuwa katika mawasiliano hayo, mtekaji alikataa katakata ombi
la kumtaka amrudishe mtoto wao na kutaka apewe kiasi cha shilingi
milioni 6 ili kutekeleza jambo hilo ingawa baadaye ilibainika jamaa huyo
alikuwa Gairo mkoani Morogoro.
Wazazi hao walisema kuwa Oktoba 19 mwaka huu mmoja wa majirani
walioguswa na tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Justin Henry
alijitolea kusafiri mpaka Gairo kumsaka mtoto na mtekaji wake jambo
ambalo lilifanikiwa kwa kumpata mtoto akiwa mzima wa afya japokuwa
mtekaji alishtukia na kukimbia.