Mgeni rasmi Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba akitoa salamu zake kwa wadau
mbalimbali (hawako pichani) waliohudhuria mkutano kabla ya kutoa hotuba yake
wakati alipokuwa akizindua rasmi Mkutano wa wadau wa uanzishwaji wa Tume ya
TEHAMA uliofanyika leo Peacock Hotels jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni
Katibu Mkuu Prof. Patrick Makungu na kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Dkt. John Mngodo.
Baadhi ya wadau mbalimbali
walioshiriki katika uzinduzi wa Mkutano wa wadau juu ya uanzishwaji wa Tume ya
TEHAMA wakifauatilia kwa makini hotuba toka kwa mgeni rasmi . Mkutano huo umefanyika
leo Peacock Hotels jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba akijibu maswali mbalimbali toka kwa
waaandishi wa habari mara alipomaliza kuzindua rasmi Mkutano wa wadau wa
uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA uliofanyika leo Peacock Hotels jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, Mhe. January Makamba (wa pili toka kushoto mstari wa mbele), wa
kwanza wake toka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia Dkt. John Mngodo. Wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za
Mawasiliano Bi. Clarence Ichwekelezwa na anayemfuatia ni Katibu Mkuu Prof.
Patrick Makungu.PICHA ZOTE
NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO.
======= ===== ======
UZINDUZI WA MKUTANO WA UANZISHWAJI WA TUME YA
TEHAMA.
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
12/09/2013.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba
amezindua rasmi mkutano wa Washikadua juu ya uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA leo
jijini Dar es Salaam.¨
Mhe.
Makamba amesema kuwa TEHAMA kitakuwa chombo kikubwa ambacho kitashirikisha
wadau wengi hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA
yanasonga mbele na inatoa fursa mbalimbali zenye kuweza kutatua changamoto za
kimaisha kwa watanzania.
Mhe.
Makamba aliongeza kuwa TEHAMA ndiyo inaleta mabadiliko na kuleta maendeleo
makubwa hivyo amesisitiza juu matumizi ya TEHAMA katika ofisi za serikali na
sekta binafsi. Aidha, amewashauri wadau wote kuangalia wenzetu nchi zilizoendelea
jinsi wafanyavyo ili kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA nchini Tanzania
yanasonga mbele. “Kama
Taifa hakuna sehemu ambapo tunakutana kutafakari juu hali ilivyo katika
matumizi ya TEHAMA hapa nchini”. Alisema Mhe. Makamba.
Kwa
upande mwingine Mhe. Makamba alisisitiza juu ya wanataaluma wa TEHAMA wawe
wanajulikana na amesema kuwa katika uundaji wa Tume hiyo ni vema wataalamu na
ufanisi wa kazi zao ujulikane ili kuepukana na kuwa na wataalamu ambao ni
Makanjanja. “Hapa
nchini Tanzania hatuna uhakika wa wahitimu katika mambo ya TEHAMA hivyo kuna
uwepo wa vyuo na tasisi ndogondogo nyingi zilizosambaa ambazo zinajikita kutoa
taaluma hiyo, katika masuala ya TEHAMA ni lazima wataalamu wajulikane na
kusajiliwa kama ilivyo katika bodi nyingine za serikali hapa nchini”. Alisema
Naibu Waziri.
Aidha,
Mhe. Makamba alimalizia kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kwa
upande wa TEHAMA kwani mpaka hivi sasa nchi imefikia mahali pazuri katika mambo
ya mawasiliano pia ameshauri juu ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika
uundaji wa tume ya TEHAMA.