Asha Baraka na wanakamati katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini Gurumo, Juma Mbizo, Cosmas Chidumule na Said Kibiriti. Kulia ni Katibu wa kamati Saidi Mdoe
.
======== ===== =====
======== ===== =====
MWANAMUZIKI
mkongwe aliyestaafu muziki akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhidini
Maalim Gurumo, ameandaliwa shoo mbili za kumuaga, moja wapo ikipangwa
kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Shoo
nyingine kwa wapenzi wote itafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika
Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na
lengo la kumuaga kwa heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya
kuyamudu maisha yake baada ya kuachana na muziki.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la
(Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki
kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa shoo hizo za kumtafutia fedha
mkali huyo.
Alisema
wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo
Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas
Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu
wa Kamati hiyo.
”Lengo
si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa
dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake
baada ya kuachana na muziki.
”Huyu
ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wakati huo, hivyo kwa sasa lazima
sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua
ataishi vipi nje ya muziki,” alisema. Naye Gurumo aliwaambia waandishi
wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki kwa sababu umri na afya yake
hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake
huo.
”Nasikia
watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena
Sikinde, jambo ambalo si kweli kwa kuwa sioni nitamuimbia nani wakati
nimechoka. ”Naomba
kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda
kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia
kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si
mahali pengine,” alisema.
Katika
hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya
kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu
ya kutambua mchango wake. ”Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya
nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake
ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema.
Kwa
mujibu wa Kamati hiyo ambayo Mdoe ndio Katibu wake, taratibu zote
zinaendelea ikiwa ni kuandaa nyimbo alizowahi kuimba na kuziweka katika
mfumo wa kibiashara, ikiwamo mpango wa kuuza nyimbo zake katika
makampuni ya simu za mikononi.