Dar
es Salaam. Mtu asiyejulikana juzi usiku alimvamia mmiliki wa maduka ya
Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad (pichani) na kumwagia maji
usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Tukio
hilo lililotokea juzi saa 1 usiku karibu na kituo cha Polisi cha
Oysterbay, lilithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Ally Mlege kwa kusema kuwa bado polisi wanaendelea na
uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika.
“Ni
kweli tukio hili limetokea ila polisi wanaendelea na uchunguzi.
Tukikamilisha uchunguzi tunatarajia kutoa taarifa kamili za tukio zima,”
alisema na kuongeza;
“Hatuna haja ya kuficha ukweli wa tukio hili, uchunguzi wetu ukikamilika na watuhumiwa wakikamatwa kila mtu atajua.”
Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizolifikia gazeti hili
zilieleza kuwa mtu huyo, alimkuta Saad akiwa anazungumza na mmoja wa
wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo karibu na Kituo cha
Polisi cha Oysterbay.
“Wakati
akizungumza na mfanyakazi wake, huyo mtu alikuwa kama anapita na
alichomoa kitu fulani na kummwagia Saad usoni na kisha kukimbia,”
zilieleza taarifa hizo na kuongeza;
“Baada
ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya AMI, sasa hatujui kama
bado yupo hapo au ameondoka, ila sisi tulizungumza naye na alitueleza
mwonekano wa mtu aliyemwagia tindikali.”
Taarifa hizo zilifafanua kwamba polisi wanazitumia taarifa hizo walizopewa na Saad, ili kuweza kumkamata mhusika.
Taarifa
hizo zilifafanua kuwa polisi wanapanga tena siku ya kumhoji kwa mara ya
pili Saad, kwamba watataka kufahamu kama mfanyabiashara huyo alikuwa
akipewa vitisho au ujumbe wowote, kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Hata
hivyo, habari nyingine zilizolifikia Mwananchi Jumapili zilieleza kuwa
mtu huyo baada ya kummwagia Saad tindikali, alipanda pikipiki na
kutokomea eneo hilo.
“Walikuwa
wawili, mmoja alikwenda kufanya unyama na mwingine alibakia katika
pikipiki, baada tu ya kumwagia tindikali mtu yule alikimbia mpaka pale
alipokuwa imesimama pikipiki, alipanda na kuondoka kwa kasi,” zilieleza
habari hizo.
Taarifa
zilizopatikana jana asubuhi zilieleza kuwa ndugu na marafiki wa
mfanyabiashara huyo, walikuwa katika mipango ya kumpeleka nje ya nchi
kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
HABARI KWA HISANI YA MWANANCHI.CO.TZ