WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Ntuchi
wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kwa kumpiga mkazi wa kijiji
cha Ifundwa wilayani hapa, Ignas Maruku (29) wakimtuhumu kuingia kwenye
bweni la wanafunzi wa kike na kuiba nguo zao mbalimbali, zikiwemo nguo
za ndani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amemweleza mwandishi wa
habari hizi kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 25 mwaka huu saa 6.00
mchana wakati wanafunzi hao wakiwa darasani.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mwaruanda
alisema siku hiyo, mmoja wa wanafunzi hao wa kike ambaye jina lake
halikuweza kufahamika mara moja akiwa nje ya madarasa karibu na bweni
lao alimwona kijana huyo akiingia bwenini mwao hivyo alimshtukia na
kuanza kupiga kelele.
Inadaiwa ndipo wanafunzi hao wa kike na
wa kiume walipotoka darasani na kuanza kumfukuza mwizi huyo kisha
kumkamata na kuanza kumshambulia kwa mawe, marungu na fimbo hadi
akazimia.
Wakati wanafunzi hao wakimsulubu mwizi
wao huyo ndipo walimu wao walipoacha shughuli zao zote shuleni hapo na
kukimbilia eneo la tukio na kuamuru wanafunzi hao watawanyike na kuacha
kumpiga mtuhumiwa huyo, warejee madarasani.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, walimu hao
walitaarifu polisi ambao kwa kushirikiana nao walimkimbiza mtuhumiwa
huyo katika Hospitali Teule ya Wilaya hiyo mjini Namanyere, lakini
alifariki dunia wakati akipata matibabu hospitalini hapo.
Kamanda Mwaruanda amedai kuwa mwalimu wa
shule hiyo aliyetambuliwa kuwa Thobias Ndunguru (26) na mkazi wa kijiji
hicho cha Ntuchi, Simon Osayi wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano
kuhusu mauaji hayo, lakini hakuna mwanafuzi yeyote anayeshikiliwa hadi
sasa huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea.
SOURCEHABARI LEO