Kamanda Wa Polisi Mkoani Mbeya |
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa
Kitongoji cha Maweni, Kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya, Flavin
Mwamosi Mwachuki (70) amepigwa hadi kufa na hatimaye kuzikwa kaburi moja
na mtu anayedaiwa kumuua kishirikina.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athuman aliyezungumza na gazeti la habari leo jana.
Alisema Mwachuki aliyekuwa mkulima na
mkazi wa Maweni alifikwa na mauti hayo juzi Ijumaa saa tisa alasiri
baada ya kushambuliwa kwa mawe hadi kufa na watu waliojichukulia sheria
mkononi, wakimtuhumu kuwa amemloga na kumuua Peter Robert (28), mkazi wa
kijijini hapo.
Kamanda Athuman aliongeza kuwa, Mwachuki
aliuawa makaburini ulikokuwa unazikwa mwili wa Robert na baada ya watu
hao kufanikisha mauaji, waliichukua miili yote na kuizika katika kaburi
moja. Kutokana na tukio hilo, Kamanda Athuman amesema msako mkali
unafanywa ili kuwabaini waliohusika na kifo cha Mwachuki.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaasa
wananchi na jamii kwa ujumla kuachana na imani za kishirikina, akisema
hazina faida zaidi ya kuchochea migogoro katika jamii zao, huku akionya
kuwa, kujichukulia sheria mkononi ni kinyume na sheria za nchi.
“Tupuuze ushirikina na tuepuke
kuwatuhumu watu na kujichukulia sheria mkononi. Kwa kuwa haya
yameshatokea, tunaomba ushirikiano wa karibu kwa watu wenye taarifa
zaidi ya tukio hili ili Jeshi la Polisi liweze kuchukua hatua za haraka
dhidi ya wahusika,” alisema Kamanda Athuman.
sourcehabari leo