KUTOKANA na uhaba wa fedha Serikalini, jumla ya wanafunzi 3,821 sawa
na asilimia 11.1 wa mwaka wa kwanza, walikosa mikopo ya kuwawezesha
kuingia elimu ya juu katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Katika mwaka huo unaoishia Juni mwaka huu, jumla ya Sh bilioni 326
zilitengwa kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi 95,902 , lakini ni
wanafunzi 30,319 pekee wa mwaka wa kwanza ndio waliokopeshwa, kati ya
wanafunzi 37,315 waliomba mkopo huo.
Hayo yalibainishwa mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo wakati akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF) aliyetaka kujua kama Serikali
imeshindwa kuwapatia mikopo baadhi ya wanafunzi wenye sifa za kuendelea
na masomo.
Akijibu swali hilo, Mulugo, alisema Serikali ina nia njema ya
kuhakikisha kila Mtanzania mwenye uwezo wa kusoma anapata fursa kusoma
katika chuo cha elimu ya Juu.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2012/2013, wanafunzi wa mwaka wa kwanza
waliowasilisha maombi ya mkopo walikuwa 37,315, lakini wanafunzi
waliokuwa na sifa ya kupata mkopo huo walikuwa 34,140, ambapo kati yao
ni wanafunzi 30,319, sawa na asilimia 88.9 ya waombaji wote, ndio
waliopatiwa mkopo huo.
“Kwa maana hiyo wanafunzi 3,821, sawa na asilimia 11.1 ya wanafunzi
wote walioomba mkopo huo, wanafunzi hawa wachache waliokosa mkopo huo
kutokana na ukomo wa bajeti pamoja na kipaumbele vya Serikali,”
alisisitiza.
Aidha, Mulugo alisema kiasi hicho cha Sh bilioni 326 katika mwaka huo
wa fedha, kimeongezeka, ikilinganishwa na kiasi cha Sh bilioni 56.1,
kilichotengwa katika mwaka wa masomo wa 2005/2006 kilichomudu kukopesha
wanafunzi 42,729.
“Ongezeko hili ni ishara tosha ya nia ya serikali kuhakikisha
wanafunzi wote wenye sifa za kusoma Vyuo vya Elimu ya Juu wanapata
mikopo,” alisema.
Pia, alisema kwa sasa Serikali inatekeleza agizo la Azimio la Bunge
la Mkutano wa 10 kwa kuwasilisha katika Bunge lijalo Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Elimu na Sheria Namba Tisa ya Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuweka utaratibu, utakaowezesha
kubaini vyanzo mbadala vya kugharamia Elimu ya Juu.
|