TASWIRA YA VIJANA WAISHIO ZANZIBAR,PICHA HII HAIUSIANI NA WALIOTAPELIWA |
ZAIDI ya vijana 130 wametapeliwa fedha
baada ya kuahidiwa ajira katika nchi za Kiarabu, ikiwemo Oman, kwenda
kufanya kazi za viwandani. Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati
akijibu hoja mbali mbali za Kamati ya Baraza la Wawakilishi, zilizokuwa
zikiwasilisha taarifa zao mbele ya Baraza.
Haroun alisema vijana hao walitapeliwa
Sh milioni 43, walizotoa baada ya kuahidiwa na wakala mmoja, kwamba
watapelekwa Oman kupata ajira za viwandani.
Alisema Wizara ilitoa hadhari mapema na
kuwataka mawakala wote wanaosafirisha vijana nje ya nchi, kuwasiliana
kwanza na Wizara, ikiwemo kuonesha mikataba ya ajira ya vijana hao ili
kupata kibali cha Serikali, kwa mujibu wa taratibu za ajira nje ya nchi.
“Wizara ilitoa hadhari mapema kuhusu
mawakala ambao hawana makubaliano na Serikali na mikataba ya kazi za
vijana huko nje ya nchi...lakini nililaumiwa pamoja na kutishiwa maisha,
kutokana na kuweka msimamo wa kuzuia vijana kwenda nje ya nchi kufanya
kazi bila mikataba,” alisema.
Haroun aliitaja kampuni ya ZAM Tours, na
kudai kwamba inahusika na utapeli huo na kuongeza kuwa wahusika mbali
mbali waliotapeliwa, wamewasilisha malalamiko yao wizarani.
Akifafanua, Haroun alisema alifuatwa na
wakala anayepeleka wafanyakazi nje ya nchi kwa ajili ya kutoa kibali,
lakini Wizara ilitaka kuona mkataba wa ajira ya vijana hao, kabla ya
kutoa kibali. Kimsingi, alisema Wizara ya Kazi na Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi na Ushirika, tayari ilikuwa katika makubaliano mazuri ya
kupeleka vijana Oman kwa ajili ya kazi mbalimbali.
Alisisitiza kuwa Wizara haina tatizo la
ajira kwa vijana nje ya nchi, lakini kwanza wanatakiwa kuwa na mikataba
ya uhakika, ikiwemo inayoonesha kazi watakazozifanya nje ya nchi.
“Msimamo wa Wizara upo wazi, tunataka
vijana wetu wafanye kazi zenye staha, zitakazozingatia heshima na utu,”
alisema. Haroun alisema hiyo ni sehemu ya masharti yaliyowekwa na
mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia ajira, ikiwemo Shirika la Kazi
Duniani (ILO).
Alikumbusha kuwa miaka ya nyuma
yalitokea matukio mbali mbali ya Wazanzibari kwenda nje ya nchi, kufanya
kazi za majumbani, hasa katika nchi za Kiarabu na baadaye kuliibuka
matatizo ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kutelekezwa.