SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amekanusha
ofisi yake kupokea rasmi ripoti ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo, na
kuiacha iozee mikononi mwake.
Amekanusha jana bungeni baada ya Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika, kuomba mwongozo, akinukuu moja ya magazeti ya
kila siku (si HabariLeo), lililoripoti kuwa ripoti hiyo imewasilishwa
kwa Spika na inaozea mikononi mwake.
Mnyika alisema katika swali lake
alilomuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Alhamisi iliyopita, alihoji juu
ya kuwasilishwa rasmi kwa ripoti hiyo na kujibiwa na kiongozi huyo kuwa
haijawasilishwa kwa Bunge.
“Sasa leo (jana) nashangaa kwenye gazeti
hili (akilionesha), limeandika Serikali yakamilisha ripoti yake, Bunge
lachambuliwa kama karanga, Ripoti yaozea mikononi mwa Spika, Serikali
yakumbushwa ya Richmond, hapa ukweli ni upi?,” alihoji Mnyika.
Alisema endapo ni kweli ripoti hiyo ya
Jairo, imewasilishwa kwa Spika na kuozea mikononi mwake, hatua hiyo
haitendei haki Bunge kwa kuwa ilitakiwa iwasilishwe bungeni na
kujadiliwa na wabunge.
Alisema na kwa mujibu wa gazeti hilo,
ripoti hiyo imelichambua Bunge kama karanga, hali ambayo Mnyika alisema
haijatoa haki kwa wabunge, kwani walipaswa kuambiwa ukweli na kupewa
nafasi ya kuijadili.
Akijibu mwongozo huo, Makinda aliikataa hoja hiyo na kusema Bunge hilo halijawahi kufanyakazi yake kwa kutegemea magazeti.
“Kwanza siikubali hoja hii, mimi kama
Spika sina taarifa hizo za kupokelewa kwa ripoti ya Jairo ofisini
kwangu, lakini pia siwezi kufanyakazi na magazeti, tena haya magazeti
ambayo mara nyingi yanaandika uongo mtupu,” alisisitiza Makinda.
Jairo alituhumiwa kuchangisha taasisi
zilizopo chini ya wizara yake Sh milioni 85, kwa madai kuwa alikuwa
anahonga wabunge ili wapitisha bajeti ya wizara hiyo katika mwaka wa
fedha wa 2011/2012.
Mnyika katika swali lake wiki iliyopita,
alitaka kufahamu sababu za Serikali kutowasilisha taarifa ya
utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na taarifa ya Kamati Teule ya
Bunge.
Alitaka kufahamu pia ni kwa nini
waliotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria, haijatekelezwa. Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alikiri Serikali kuzembea katika kutoa mrejesho kuhusu
suala hilo na kusema kuwa sehemu kubwa ya maazimio hayo yamefanyiwa
kazi.
- Imeandikwa tarehe 30 Aprili 2013
- By Halima Mlacha, Dodoma