VIINI SUGU VYA MALARIA VYAGUNDULIWA

Mmbu wanaosababisha Malaria

Aina mpya ya viini sugu vinavyosababisha Malaria na ambavyo havisikii dawa vimegunduliwa na wanasayansi.
Watafiti wamevigundua viini hivyo Magharibi mwa Cambodia na wanasema kuwa vina umbo tofauti la genetiki ikilinganishwa na viini vingine duniani.
Viini hivi ni sugu kiasi cha kutosikia dawa aina ya Artemisinin, dawa yenye nguvu zaidi katika kutibu Malaria.
Taarifa ya kwanza kuwa wagonjwa walikuwa hawatibiki na dawa hiyo ilitokea mwaka 2008. Tatizo hilo tangu hapo limeenea katika maeneo mengine ya Asia ya Kusini.
Utafiti huu umechapishwa katika jarida la ''Nature Genetics.''
Mtafiti mkuu Daktari Olivo Miotto, wa chuo kikuu cha Oxford na kile cha Mahidol nchini Thailand,amesema kuwa dawa zote zenye uwezo wa kuua Malaria na ambazo zimevumbuliwa katika miaka ya hivi karibuni, zimekuwa ovyo katika kutibu Malaria.
"Dawa ya Artemisinin kwa sasa inafanya kazi vyema. Ndio silaha nzuri zaidi dhidi ya ugonjwa huo na tunahitaji kuendelea kuitumia,'' alisema Daktari Miotto
Magharibi mwa Cambodia kumetajwa kama sehemu yenye Malaria sugu.
Haileweki ni kwa nini tangu mapema miaka ya 1950, viini vya Malaria katika eneo hilo, vimekuwa sugu. Tatizo hilo pia limesambaa hadi katika sehemu kadhaa za Asia na Afrika.
Kwa sasa wanasayansi wana wasiwasi kuwa hali sawa na hiyo itajitokeza kwa dawa ya Artemisinin. Dawa hiyo inatumika kote duniani kukabiliana na Malaria, na inaweza kutibu ugonjwa kwa siku chache tu ikiwa itatumika na mchanganyiko wa dawa zengine.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family