WASOMI 200 waliojitolea kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka jana, ujasiri wao umezaa matunda mema. Hali hiyo imetokana na kutambuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ameutaka uongozi wa Jeshi hilo kuwaajiri ili wasipotee na utaalamu wao baada ya kumaliza mkataba wa mafunzo.
Akizungumza katika makao makuu ya JKT, Dar es Salaam jana alipofanya ziara ya kikazi, Rais aliyeweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza kutembelea eneo hilo akiwa madarakani alisema, kujitolea kwa wasomi wenye Shahada na shahada za uzamili kushiriki mafunzo ya JKT ni heri, hivyo wasiachwe wakapotea.
“Matarajio yetu katika Operesheni Sensa yetu ya mwaka 2012 yalikuwa kupata watu wasio na elimu na walio na elimu ya kati, lakini cha kufurahisha ni kwamba hata wenye Shahada na Shahada za Uzamili nao walijitokeza kwa wingi na kumaliza vizuri mafunzo ya awali ya kijeshi kwa miezi sita. Hao 200 si haba.
“Nimekuwa nikipata ujumbe wao kwamba wamemaliza mafunzo ya awali na mwingine niliupata jana (juzi) wanauliza: ‘Sasa tumemaliza mtatuacha tu?’ Nimewajibu kwamba mimi si mwajiri, lakini kwa sababu mwajiri yupo hapa mkutanoni, ninawaletea suala hili, fanyeni utaratibu muwaajiri kulingana na fani zao watawafaa, hivyo msiache wakarejea nyumbani na kuwapoteza,” Rais alisema.
Akisisitiza hoja hiyo, alisema si lazima wote waajiriwe JKT bali hata kwenye maeneo mengine ya Jeshi nchini.
“Cha msingi JKT iangalie ni idadi gani inahitaji na wengine mwajiri ataangalia mahali pa kuwapangia kazi kulingana na uwezo wao wa kiutendaji na elimu. Mafunzo mengine yanaweza kufuata wakiwa ndani ya ajira,” Rais alisema.
Alifafanua, kuwa mkataba wa miaka miwili waliouingia na JKT kimafunzo, usiachwe ukaisha kwani kuwapata baada ya hapo inaweza kuwa kazi itakayoilazimu JKT kuwatafuta wengine kwa kuwalazimisha ili wajiunge na Jeshi hilo.
Wakati huo huo, Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa JKT itaanza rasmi Machi 4, ikiwa na lengo la kutimiza majukumu yaliyokuwa yakitimizwa na lililokuwapo kabla ya kufutwa mwaka 1994.
Hata hivyo, tofauti na matarajio, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Muhuga alimweleza Rais kuwa uwezo wa kifedha uliopo ni mdogo kuhudumia watu wachache katika kambi zote nchini.
Kwa mujibu wa Muhuga, kinyume na ilivyokuwa katika JKT ya awali kwamba wahitimu wote wa kidato cha sita wanajiunga na JKT kwa lazima, kati ya 41, 000 waliomaliza kidato hicho mwaka huu, ni 5,000 tu ndio watajiunga kwa lazima huku 5,000 wengine wakitoka katika kundi la hiyari la vijana na wabunge 47 watakaokuwa kambini kwa wiki tatu.
“Hali ya majengo yetu si nzuri na uwezo wa kuhudumia watu wengi hatuna kwa sasa, kutokana na hilo, idadi ya wanaopaswa kuingia JKT kwa hiyari na kwa kujitolea inatuzidi uwezo,” alisema na kuongeza kuwa wamelazimika kutumia vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu ili kuchagua wahitimu wa kidato cha sita watakaojiunga.
Wawekezaji Baada ya kuelezwa kuhusu uzalishaji mdogo wa mbegu na mahindi, Rais alitoa mwito kwa viongozi wa JKT waingie ubia na raia au wawekezaji wenye utaalamu wa uzalishaji katika maeneo wasiyo na utaalamu nayo.
“Wapo raia wenye uwezo na utaalamu wa kilimo na ufugaji, watafuteni mwingie ubia ili mfanye uzalishaji wenye tija. Kuna maeneo hayahitaji kuendeshwa kijeshi bali kwa kuzingatia utaalamu, sasa itakuwa vizuri kama mtashirikisha wataalamu wawasaidie kuyaendesha kwa faida, mkitafuta wababaishaji mtaishia kushitakiana mahakamani na msipoangalia, mtajikuta mnashindwa,” aliasa.
Madeni SUMA JKT Katika hatua nyingine Rais alielezwa kuwa shirika hilo limefanikiwa kukusanya Sh bilioni 16 kati ya Sh bilioni 58 linazodai kutoka kwa wateja waliokopeshwa matrekta, lakini Rais alitoa angalizo kwamba Serikali haitakuwa tayari kuona inapoteza fedha hizo, kwa kuwa haikulidhamini shirika hilo kwa lengo la kutoa msaada au ubani kama inavyofanya kwenye misiba.
“Ni lazima madeni yote yakusanywe, kwa sababu muda utafika wakati mkopeshaji kutoka India atatakiwa kulipwa Sh bilioni 40 zake, zilizobaki kwa wateja ni Sh bilioni 42, ambazo hatuko tayari kuzilipa kupitia jasho la walipa kodi. Waliochukua matrekta wakumbushwe ili walipe,” Rais alisema.
Kuhusu madeni ya mbegu bora ya Sh milioni 420 ambayo JKT inadai kampuni tatu akiwamo Wakala wa Mbegu wa Taifa, Rais alisema ‘atamvaa’ wakala huyo wa Serikali ili alipe na kwamba kampuni mbili binafsi; Tropical Seeds na Highlands Seeds, watapaswa kufuatiliwa na waliowakopesha. Mapigano Tarime Rais Kikwete aliitaka JKT ihakikishe uwepo wake katika uwanja unaotumiwa kwa mapigano Tarime kati ya Waanchari na Warenchoka unakuwa chachu ya amani na si uzalishaji pekee.
“Wale watu wakishachokozana huko wanabebana hadi kwenye uwanja ule na kuanzisha mapigano, wala hawagombei eneo hilo sasa ninyi mmepewa mlitumie kwa uzalishaji na ujenzi, hakikisheni uwepo wenu unamaliza mapigano hayo,” alisema.