MTENDAJI MKUU WA MAMLAKA YA RELI TANZANIA NA ZAMBIA(TAZARA) AACHIA NGAZI

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA) Bw.
Akashambatwa Mbikusita-Lewanika,
hatimaye ameachia ngazi baada ya
kuendesha kampeni kali ya miezi kadhaa
kutaka aendelee kuongoza Mamlaka hiyo
kwa miaka mingine mitatu.
Hatua hiyo ya kuachia ngazi imekuja baada
ya Bodi ya Wakurugenzi na Baraza la
Mawaziri la Mamlaka hiyo kuonyesha
dhahiri kutotaka Mzambia huyo aendelee
na uongozi wa TAZARA kutokana na
utendaji wake mbovu na uongozi mbaya
uliowabagua wafanyakazi wa Mamlaka
hiyo kwa misingi ya utaifa wao.
Habari za ndani za Mamlaka hiyo
zimesema Bw. Akashambatwa ambaye
kipindi chake cha uongozi kiliisha tarehe
22 Januari, 2013 kiliongezwa kwa maombi
maalum ya Serikali ya Zambia kwamba
Serikali hiyo ilihitaji muda mrefu kidogo
kumpata mbadala wake, licha ya Serikali
ya Tanzania kutoridhishwa na utendaji
wake.
Katika kikao chake cha tarehe 20 Februari,
2013 jijini Lusaka, Zambia, Baraza la
Mawaziri lilijadili kwa siri na kwa kirefu
suala la mtendaji Mkuu huyo ambaye
inasemekana aliombewa tena na Serikali
ya Zambia kipindi cha nyongeza, ombi
ambalo inadaiwa lilipingwa vikali na
ujumbe wa Serikali ya Tanzania
ukiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe.
Taarifa za uhakika ndani ya Wizara ya
Uchukuzi zinasema Serikali ya Tanzania
haikumtaka Mtendaji Mkuu huyo kwa
sababu kadhaa zikiwemo :uwezo mdogo,
ubadhirifu, kuchochea ubaguzi kati ya
Watanzania na Wazambia, ukaidi na
uchochezi. Inadaiwa kuwa Mtendaji Mkuu
huyo alizuia kuanzishwa kwa mradi wa
usafiri jijini Dar es Salaam bila sababu
yoyote ya msngi na kuishia kusambaza
taarifa za uongo na uchochezi Zambia na
magazeti mbalimbali nchini.
Tarehe 25 Februari, 2013 Gazeti la kila
siku la Zambia, Zambia Daily Mail, liliripoti
tukio hilo la kuachia ngazi kwa kiongozi
huyo ambaye anajulikana sana nchini
Zambia kama mfanyabiashara na kiongozi
wa kimila (chief),
Gazeti hilo lilinukuu barua ya Bw.
Akashambatwa ya tarehe 22 Februari,
2013 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Uchukuzi, Ujenzi, Ugavi na Mawasiliano
ya Zambia, akielezea kuwa hakuna faida
ya kuomba kurefushwa kwa mkataba
wake wakati vyombo vikuu vya uongozi
vya TAZARA, Bodi ya Wakurugenzi na
Baraza la Mawaziri, havionyeshi
kumkubali.
Kuondoka kwa Bw. Akashambatwa
kwenye uongozi wa TAZARA kunatarajiwa
kupokewa na wafanyakazi wa TAZARA kwa
nderemo na vifijo.

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family