Baraza
la mitihani la Taifa, NECTA, limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato
cha nne uliofanyika mwezi November mwaka jana, huku kiwango cha ufaulu
wa masomo ukipanda kati ya asilimia 0.16 na 16.72 ikilinganishwa na
mwaka 2012, na wasichana wakiibuka kidedea katika ufaulu wa jumla kitaifa. Jumla ya watahiniwa 235,227 sawa na asilimia 58.25 ya watahiniwa wote wamefaulu mtihani, idadi ya wasichana ikiwa 106,792 na wavulana 128,435, tofauti na mwaka 2012 ambapo waliofaulu walikuwa ni 185,940. Kaimu katibu mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde anatangaza rasmi matokeo haya, ambayo yanaonyesa ufaulu kimasomo ukiongozwa na somo la Kiswahili, kwa asilimia 67.77 huku somo la hisabati likiendeleza historia ya kushika mkia, kwa ufaulu wa asilimia 17.78. Kati ya watahiniwa kumi bora waliofanya vema kitaifa, saba kati yao ni wasichana wakitokea shule za Marian girls, St. Francis Girls na Cannossa. Lakini ni viwango vipi vimetumika katika usahihishaji wa mtihani huu, kwa kuzingatia mkanganyiko uliojitokeza kuhusiana na madaraja ya ufaulu? Aidha, NECTA imefuta matokeo yote ya mtihani kwa watahiniwa 10 waliobainika kuandika matusi katika karatasi zao za majibu, na adhabu hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 6(2)(a) cha kanuni za mtihani. Aidha baraza hilo limefuta matokeo yote ya mtihani kwa watahiniwa 272,waliobainika kufanya udanganyifu kwa njia mbalimbali, ambapo watahiniwa 242 ni wa shule, 19 ni watahiniwa wa kujitegemea na 11 ni wale wa maarifa ama QT. Shule zilizojitokeza kufanya vizuri zaidi ni Marian wasichana na wavulana, St. Francis wasichana, Anne Maria, Kizirege, Cannossa na shule ya mwisho kwa kigezo cha watahiniwa zaidi ya 40 ikiwa ni Kitonga na chini ya watahiniwa 40 ikiwa ni shule ya Uchindile ya Morogoro. |