Mshambuliaji
wa kimataifa mtanzania anayekipiga TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, Mtanzania Mbwana Samatta, amesema Mrisho Ngassa
wa Yanga amefanya kitu cha maana kwa kupiga ‘Hat-Trick’ mbili mfululizo
kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Samatta alisema idadi hiyo ya mabao si kazi rahisi kwenye mashindano makubwa kama hayo.
Yanga iliifumua Komorozine ya Comoro mabao 12-2 na kuiondosha kwenye
mashindano na sasa itaikabili Al Ahly ya Misri ambayo Samatta amesema si
timu ya ajabu lakini si laini kama hakuna mipango ya maana.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka Lubumbashi, Samatta
alisema: “Mabao sita ni mengi sana kufunga katika Ligi ya Mabingwa
Afrika, ni dalili nzuri kwake na kwa timu.
“Pia yanaashiria mambo mazuri kikubwa, lakini asibweteke kwani
anaweza kufanya kitu kikubwa katika mashindano hayo endapo Yanga
itafanikiwa kusonga mbele.
“Ngassa ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu, kwangu sioni kitu cha
ajabu sana kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja kwa sababu nafahamu
uwezo wake, lakini inaashiria pia kwa sasa yuko vizuri sana kimwili na
kiakili.”
Kuhusu Yanga na Al Ahly, Samatta alisema: “Al Ahly ni timu kubwa na
kama ulivyoona ni mabingwa, lakini mpira ni mchezo wa ajabu, nina imani
kama Yanga watajituma, wanaweza kuwavua ubingwa na wao wakasonga mbele.”
Mazembe nayo imo kwenye michuano hiyo na inajiandaa na mechi dhidi ya
Astres de Douala ya Cameroon. Kuhusiana na mchezo huo, Samatta ameweka
wazi kuwa maandalizi yao ni ya nguvu.
|