Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' kimeondoka jana jioni kwenda nchini Kenya kwa ajili ya mashindano ya Chalenji kikiwa na lengo moja la kutwaa ubingwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati timu hiyo ikikabidhiwa Bendera ya Taifa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania, Henry Lihaya, Kocha mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen alisema wanaondoka nchini wakiwa na nia ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, lakini lengo lake la kwanza ni kuhakikisha timu hiyo inafuzu kutoka hatua ya makundi na kuingia hatua ya mtoano.
Alisema baada ya kuvuka hatua hiyo lengo lake la pili ni kupambana vilivyo ili kuhakikisha wanaibuka mabingwa wa mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka 1994, ambapo timu hiyo ilinyakua kombe hilo nchini Kenya.(P.T)
Katika mashindano hayo, Kilimanjaro
Stars ipo kundi B na timu za Zambia, Burundi na Somalia, ambapo itacheza
mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia, Novemba 28 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Machakos.
Poulsen alisema anaamini kuwa
watakumbana na ushindani mkubwa, lakini hiyo ndiyo itakuwa nafasi kwa
wachezaji wake kupigana vilivyo na wale chipukizi ndiyo wakati wao wa
kumwonyesha kuwa wanaweza. Pia hii ndiyo tiketi ya kujitangaza kimataifa
wakati wale wakongwe ndiyo muda wao wa kumwonyesha kuwa wanastahili
kuendelea kubakia katika kikosi hicho na kile cha Taifa Stars.
"Pia mashindano hayo nitayatumia kwa
ajili ya kuangalia wachezaji watakaounda kikosi cha Taifa Stars kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar ambao wataiwakilisha Tanzania katika harakati
za kutafuta tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Afrika 2015," alisema
Poulsen.
Naye Lihaya aliwataka wachezaji wa
Kilimanjaro Stars kwenda kupambana na kuhakikisha wanafanya vizuri na
kurejea nchini wakiwa na kombe.