*Mazungumzo ya Uganda yakwama tena, Bisiimwa asema yeye si mtu rahisi
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
KIKUNDI cha waasi wa M23, jana asubuhi kimeanzisha upya mapigano dhidi ya Jeshi la Serikali ya Kongo (FARDC), linaloshirikiana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO), katika eneo la Mashariki mwa mji wa Goma, RAI Jumapili limedokezwa. (HM)
Mashambulizi hayo ya waasi wa M23
yamekuja saa chache baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani usiku wa
kuamkia jana, yaliyokuwa yakifanyika mjini Kampala, Uganda, chini ya
Mwenyekiti wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Rais Yoweri
Museveni.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana
kutoka kwa chanzo chake kinachoaminika, kilichoko uwanja wa mapambano
nchini Kongo, zilieleza kuwa waasi hao wameanzisha mashambulizi ya
kurejesha himaya zao zilizopo katika mji wa Rumangabo, ambazo
walipokonywa hivi karibuni na Jeshi la Congo (FARDC).
"Kwa sasa nipo kwenye eneo la Milima
ya Kinyori, ambayo inapatikana karibu na mpaka wa Rwanda na Uganda, huku
mashambulizi ni makali, ninachokiona hapa ni helikopta ya kivita ya M23
ikijiandaa kuruka kwa ajili ya kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na
wanajeshi wa FARDC," kilisema chanzo chetu hicho.
Wakati hayo yakijiri, zipo taarifa
zinazoeleza kuwa ndege ya kijeshi ya Serikali ya Kongo juzi ilianguka na
kulipuka moto, wakati ikijaribu kutua katika Uwanja wa Ndege wa
Bangoka, uliopo mkoani Ituri.
Kwa mujibu wa habari zilizolifikia
gazeti hili, ndege hiyo ilikuwa imebeba silaha za kivita, lakini bado
haijajulikana mara moja chanzo cha ajali yake.
Wakati huo huo, habari ambazo gazeti
hili limezinasa kutoka nchini Uganda kulikokuwa kukifanyika mazungumzo
ya kuleta amani nchini Kongo, zinaeleza kuwa kwa mara nyingine waasi wa
M23 na Serikali ya Kongo wameshindwa kuafikiana na hivyo mazungumzo
yaliyokuwa yakiendelea yamevunjika usiku wa kuamkia jana.
Inaelezwa kuwa kuna mambo matatu ambayo yamesababisha kuvunjika kwa mazungumzo hayo.
Mambo hayo ni pamoja na Serikali ya
Kongo kutakiwa kukubali kutoa msamaha kwa makamanda wa waasi wa M23,
jambo ambalo lilikataliwa na upande wa serikali, kwa madai kuwa
makamanda hao wanashutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa makosa ya jinai,
ikiwamo kuwatumikisha watoto kijeshi, kutekeleza mauaji pamoja na
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Sharti la pili ambalo lilisababisha
mvutano na hivyo kushindwa kufikia muafaka ni lile la kuitaka Serikali
ya Kongo iwajumuishe wapiganaji wa M23 katika Jeshi la Serikali (FARDC),
ambapo kwa upande wa serikali ulishauri kwamba wapiganaji wa M23
washushe silaha zao chini, halafu wajikusanye katika kambi moja ya
kijeshi, jambo ambalo lilipingwa vikali na viongozi wa M23.
Kwa upande wa sharti la tatu, waasi wa
M23 walitaka viongozi wao wajumuishwe katika Serikali ya Kongo, hata
hivyo Serikali ya Kongo imegoma kwa madai kwamba viongozi wa serikali ya
nchi hiyo hutokana na demokrasia ya kupigiwa kura na wananchi, hivyo
wakahoji M23 watakuwa wamepigiwa kura na nani?
Kabla ya kuvunjika kwa mkutano huo,
RAI Jumapili ilifanya mahojiano kwa njia ya simu toka nchini Uganda na
Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa, ili atoe ufafanuzi wa taarifa tata
zilizomhusisha na kujisalimisha kwa jeshi la Uganda (UPDF).
Kiongozi huyo alikanusha taarifa hizo na kusema kuwa yeye hawezi kamwe kujisalimisha na kwamba si mtu rahisi kukamatwa.
Akizungumzia wapiganaji wake
kuchakazwa vikali na jeshi la Serikali ya Kongo, likishirikiana na
kikosi maalumu kinachoundwa na Umoja wa Mataifa cha Force Intervention
Brigade (FIB) usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii na kusababisha kukimbia
ngome yao ya Rumangabo, Bisiimwa alisema hawakukimbia mapigano, ila
walirudi nyuma kwenye uwanja wa mapigano ili kutoa nafasi ya mazungumzo
ya amani yanayofanyika mjini Kampala.
"Nipo kwenye mkutano mjini Kampala,
kwa hiyo sina muda wa kuongea kwa kirefu, sisi hatujakimbia, ila
tumetoka katika mstari wa mbele wa mapambano ili kupisha mazungumzo
haya...nashangaa habari zilizoenezwa kwamba nimejisalimisha kwa jeshi la
Uganda, kwa nini nifanye hivo, mimi si mtu wa kukamatwa kirahisi,"
alisema Bisiimwa.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo
wa M23 alikanusa habari za kumeguka kwa kundi lake na kuunda kikundi
kipya cha waasi kilichoanzishwa hivi karibuni, kinachojulikana kwa jina
la M18.
Bisiimwa alisema kikundi hicho
anakisikia tu, kwamba kipo katika Mkoa wa Ituri, ambao upo Kivu
Kaskazini, eneo ambalo lipo mbali sana na sehemu ambayo vikosi vya M23
vinatawala.
Waasi wa M23 walikuwa wamejizatiti
katika kambi zao tatu zilizopo katika mji wa Rumangabo, ambao
unapatikana kilomita 50 kutoka mji wa Goma, baada ya kuzidiwa nguvu na
kufurumushwa katika mji wa Goma na FIB kwa kushirikiana na Jeshi la
Serikali ya Kongo Agosti, mwaka huu.
Baada ya mashambulizi makali
yaliyofanywa na Jeshi la Serikali ya Kongo Jumatano ya wiki hii, waasi
hao waliukimbia mji wa Rumangabo na kutokomea katika milima ya Mbuzi,
Chanzori, Kinyori na Chanzi. Chanzo: mtanzania