Afisa Habari Mwandamizi toka
Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Bi. Prisca Ulomi(kushoto)
akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu Uanzishwaji wa
Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, wakati wa Mkutano
uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Jijini Dar Es
salaam.Kulia ni Afisa Habari Idara ya Habari(MAELEZO) Hassan
Silayo.Picha na Eliphace Marwa
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAWASILIANO, SANYANSI NA TEKNOLOJIA
1. Napenda
kuchukua fursa hii kuwashukuru wote mliofika katika mkutano huu muhimu
wenye lengo la kuwaelimisha wananchi na wadau wa Sekta ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhusu umuhimu wa kuundwa kwa Tume ya
kitaifa ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini. Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni moja kati ya Sekta zinazokua kwa
kasi hapa nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika
maendeleo ya Taifa na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na
kuboresha maisha ya wananchi na huduma za jamii kwa ujumla.
Kutokana na
ukuaji wa Sekta hii, jitihada za makusudi zinahitajika katika kusimamia
na kuratibu shughuli za TEHAMA ili nchi iweze kunufaika zaidi kwani
mchango wa sekta hii unaweza kuwa mkubwa kama TEHAMA na matumizi yake
yataratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema zaidi kuliko hali ilivyo
sasa. Katika kuhakikisha masuala ya TEHAMA nchini yanaratibiwa,
kusimamiwa na kuendelezwa vyema, Serikali iliona ni vema ikaundwa Tume
ya TEHAMA (ICT Commission). Uamuzi huu pamoja na mambo mengine,
unatambuliwa na Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 ambayo pia
inaelekeza kuundwa kwa chombo cha TEHAMA ikiwemo juhudi na program
mbalimbali zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji utaratibu wenye
ufanisi. Aidha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inaendelea
na taratibu za uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA ikiwepo juhudi na program
mbalimbali zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji uratibu wenye
ufanisi.
Kwa kutambua
mchango wa wadau katika ukuzaji wa sekta ya Mawasiliano nchini, wadau
mbalimbali wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wamehusika
na kushiriki kikamilifu kutoa maoni katika hatua zote za uanzishwaji wa
Tume hii. Tume hii inalenga kutambua na kuvutia fursa za uwekezaji
katika TEHAMA, kutoa ushauri, kuendeleza rasilimali watu kitaifa kwenye
sekta ya TEHAMA, kuendeleza program za kitaifa za TEHAMA na kushiriki
katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ya TEHAMA yenye sura ya kitaifa
kwa kushirikisha wadau wa sekta zote.
2. Jitihada
za kuanzisha Tume zinalenga kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja
na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo maagizo ya
Mkutano wa Dunia wa Jamii Habari (World Summit on Information Society).
Aidha, jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha
Sekta ya TEHAMA inakua nchini. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na
uanzishwaji wa vituo vya Mawasiliano vya Jamii (community telecentres),
ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband
Backbone-NICTBB), Uanzishwaji wa Wakala wa Serikali Mtandao, Uanzishwaji
wa Vituo vya Kutunzia kumbukumbu za TEHAMA (Data centres), na Mradi wa
Anwani za Makazi na Simbo za Posta (Physical Adressing System and
Postcode)
3. Mafanikio
katika jitihada hizi yamekabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo
kutokuwepo kwa chombo mahususi kinachoratibu, kusimamia na kuendeleza
TEHAMA nchini. Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano inakuwa kwa kasi
kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu, na hivyo kufanya baadhi ya
mambo kuwa na changamoto katika utekelezaji wake hususan kutokuwepo na
uratibu wa kitaifa katika miradi na program zenye sura ya kitaifa. Pia,
kukosekana kwa mpango wa Kitaifa wa usimamizi wa kuhakikisha kuwa
mifumo ya TEHAMA inawasiliana na hatimaye kuepuka upotevu wa rasilimali
unaotokana na taasisi mbalimbali kufanya kitu kile kile (duplication of
efforts); Changamoto nyingine ni kutokuwapo na usimamizi, usajili wa
kitaifa wa kuendeleza weledi kwa wataalamu wa TEHAMA (professional
development, registration and certification) na kuhakikisha utoshelevu
wa rasilimali watu utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya TEHAMA;
Kutokuwepo chombo mahususi chenye majukumu ya kisheria.
4. Tume
hii inatarajia kuondoa changamoto hizo tajwa hapo juu na kujenga mfumo
utakaowezesha uwekezaji wa kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano na TEHAMA yenye sura ya kitaifa; Kuwepo mfumo
utakaowezesha wabunifu na wajasiriamali kuendeleza sekta ya TEHAMA; na
kuweka utaratibu na miongozo ya namna bora ya kuhifadhi vifaa chakavu
vya TEHAMA (e-waste management).
5. Tume
ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano itasaidia kukuza uchumi wa Taifa
kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na kuchochea uzalishaji, ukuaji wa
sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma za jamii; kuwa na taifa
la jamii Habari, lenye wataalam wanaotambulika kitaifa na kimataifa, na
wajasiriamali katika Nyanja mbalimbali za TEHAMA kuendana na kasi ya
ukuaji wa teknolojia duniani; kuwa na uhakika wa usalama katika matumizi
ya TEHAMA na kuwepo na mfumo unaoainisha na kuendeleza uwekezaji katika
sekta ya TEHAMA kitaifa.
6. Kwa
niaba ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia napenda kuchukua
fursa hii kuwashukuru wadau na wananchi wote wanaoshiriki kwa njia moja
au nyingine katika uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA nchini.
Imetolewa na;
Prisca J. Ulomi
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.