Vijana wa Scout wakimvisha skafu Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete muda
mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mafia jana asubuhi
ambapo alifungua uwanja wa ndege wa Mafia na kuzindua Gati la Mafia.Rais
Kikwete yupo katika ziara ya kikazi ya mkoa wa Pwani.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa kuashiria kuzindua
rasmi uwanja wa Ndege Mafia uliojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali
ya Tanzania na mfuko wa Millenium Challenge Corporation (MCC), Kulia ni
Mratibu wa shughuli za MCC nchini Bwana Bernard Mchomvu na katikati ni
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi Mwantumu Mahiza na Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete
Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na baadhi ya wananchi wa wilaya
ya Mafia muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi Gati la Mafia jana
asubuhi.Picha na Freddy Maro-IKULU
---
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Ni kero za miaka mingi za wananchi wa Mafia
· Awaambia kuwa Serikali sasa imetimiza ahadi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
jana, Alhamisi, Oktoba 3, 2013 amezindua miradi miwili mikubwa ya
maendeleo Kisiwani Mafia ambayo inamaliza kero za miaka mingi za wakazi
wa Kisiwa hicho.
Rais
Kikwete amezindua Uwanja wa Kisasa wa Ndege wa Mafia na pia amefungua
Gati ya Mafia, miradi mikubwa ya miundombinu iliyoko mjini Kilindoni na
ambayo inamaliza malalamiko ya miaka mingi ya usafiri ya wakazi wa
Mafia.
Ndege
iliyombeba Rais Kikwete imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mafia kiasi
cha saa 5:35 asubuhi na kuanza mara moja shughuli ya kuzindua Uwanja huo
ambao umejengwa kwa gharama za dola za Marekani milioni 13.57.
Uwanja
wa Ndege wa Mafia ni moja ya miradi mingi na mikubwa ya miundombinu
inayotekelezwa nchini chini ya misaada ya Shirika la Misaada ya
Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) na ambayo katika Tanzania utekelezaji wake uko chini ya Akaunti ya Changamoto za Milenia Tanzania ya Millennium Challenge Corporation Tanzania (MCA(T).
Hiyo
ndiyo imekuwa shughuli ya kwanza kufanywa na Rais Kikwete ambaye
ameanza ziara ya siku tano ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo
katika Mkoa wa Pwani kwa kutembelea Kisiwa cha Mafia.
“Bado
tunayo kazi ya kufanya kuhusu uwanja huu wa Mafia ikiwa ni pamoja na
kuuwekea taa, ili uweze kutumika hata usiku, na pia kujenga jengo jipya
la kisasa la abiria ili kuongeza uwezo wa usafiri wa Kisiwa cha Mafia
kuliko ilivyo sasa,”
amesema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Najua
kuwa wakazi wa Mafia, kwa miaka mingi mmekuwa na vilio viwili vikubwa
vinavyohusiana na miundombinu, usafiri na mawasiliano ya usafiri – yaani
uwanja wa ndege na gati. Yote mawili sasa tumeyafanikisha na
kuyatekeleza kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka
2013. Ndugu zangu wa Mafia kimebakia nini sasa?” amesema Rais Kikwete na kuelezea jitihada za Serikali za kujenga viwanja vya ndege nchini.
Kwenye
Bandari ya Kilindoni, Rais Kikwete amezindua Gati ya Mafia ambayo ina
urefu wa kilomita 1.3, uwezo wa kubeba magari yenye tani zisizozidi 10
na yanayokwenda kwa kasi ya maili 15 kwa saa, mradi ambao umegharimu
kiasi cha Sh. bilioni 20.
Baada
ya kuzindua rasmi Gati hiyo, Rais ametembea urefu nzima wa daraja hilo
ambako aliwapokea abiria wa kwanza kutumia Gati hiyo na kuwasalimia
wafanyakazi wa Meli ya F.B. Khadija ambayo itakuwa inatoa huduma kati ya
Mafia na Nyamisati, Mkoa wa Pwani pia.
Akizungumza
na mamia ya wananchi waliohudhuria shughuli za ujenzi huo, Rais Kikwete
amefurahi kuwa Serikali yake imeweza kumaliza kero mbili kubwa na za
muda mrefu ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi wa Mafia.
Rais
Kikwete ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambayo imejenga na
inamiliki Gati hiyo kuweka usafiri wa kuwavusha wasafiri kutoka Gatini
hadi meli zinapoegeshwa na kutoa changamoto kwa Mamlaka hiyo sasa
kujenga Bandari kamili hapo hapo Mafia.
Rais
Kikwete amerejea Dar es Salaam jioni ya leo na kesho ataendelea na
ziara ya Mkoa huo wa Pwani kwa kutembelea Wilaya ya Mkuranga.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
3 Oktoba, 2013