Wanawake nchini Saudi Arabia wamekaidi sheria inayowapiga
marufuku kuendesha gari. Siku ya Jumamosi wanawake kadhaa Saudi
walionekana wakiendesha magari pamoja na kuwepo tishio la kuadhibiwa
vikali. Ripoti zinasema kuwa Wasaudi 17 elfu wametia saini waraka wa
intaneti wa kuunga mkono haki ya wanawake kuendesha gari. Bi. Manal
al-Sharif mmoja wa wanaharakati walioratibu shughuli hiyo jana anasema
serikali imemuonya ikisema itamchukulia hatua kali.
Saudi Arabia ndio nchi pekee ulimwenguni ambayo wanawake hawana
ruhusa ya kuendesha magari, suala ambalo linatokana na fatuwa za
wanachuoni wa Kiwahabi wa nchi hiyo. Iwapo mwanamke yeyote atatiwa
mbaroni mwa kosa la kuendesha gari, adhabu yake ni kuwekwa korokoroni,
kufunguliwa mashtaka mahakamani na hata kupigwa bakora.