Kamati ya bunge inayohusika na
ulinzi na uhusiano na mataifa ya kigeni imependekeza kufungwa kwa kambi
za wakimbizi nchini Kenya, ikisema zinatishia usalama wa nchi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndungu Githinji
amesema kuwa wana habari kuwa kambi zilizoko kwenye mipaka ya Kenya
hutumika kuwapa mafunzo wapiganaji wa kiislamu.Kenya inahifadhi wakimbizi wa kisomali zaidi ya nusu milioni katika kambi za Dadaab zilizoko kwenye mpaka na Somalia.
Mwenyekiti huyo Ndungu Githinji ameambia BBC kuwa miaka 22 imetosha kwa usaidizi kwa wasomali hao na wanastahili sasa kurudi nyumbani baada ya amani kurejeshwa nchini mwao.
''Hawa wakimbizi wamekaa miaka ishirini na mbili Kenya. Ningependa kuuiomba UN ifunge kambi hizo. Iwarudishe wasomali kwao, maana sasa nao pia wanayo serikali yao. Ili tuweze kukaa kwa amani.''Amesema bwana Githinji.
Lazima usalama uimarishwe
Bwana Githinji pia ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuzidisha usalama na doria katika maeneo yanayotishiwa kushambuliwa na Al shabaab.''Tunasikia AL shabaab wanasema kwamba bado wanataka kutupiga. Naomba kuwa zile sehemu zote walizotoshia kushambulia zipewe ulinzi wa kutosha kwa saa ishirini na nne.''
Wanamgambo wa Alshabaa wamekuwa wakijihusisha na waislamu katika harakati zao huku wakidai kuwa wanapigania haki ya dini ya kiislamu nchini Somalia na hata mataifa jirani kama vile Kenya.
Pia wamekuwa wakilenga Kenya kwa mashambulio kufuatia hatua ya Kenya kuingia nchini Somalia mwaka wa 2011 kuwaondoa wanamgambo hao kwa madai kuwa wanatishia usalama wa nchi.
Kutokana na hilo wabunge waliozuru eneo la shambulio kule Westgate wamefurahishwa na hatua ya waislamu nchini Kenya kujiepusha na kundi hilo la AL-Shabaab.
Mwenyekiti Githinji asema, '' Ningependa kupongeza viongozi wa waislamu ambao wametoa taarifa yao kuwa hawaungi mkono mashambulio haya.''
Mwandishi wa BBC jijini Nairobi anasema kuwa wito huu wa kufungwa kwa kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma, zimekuwepo kwa muda. Wakenya wengi wanahisi kuwa Kuwepo kwa wakimbizi hao kumeendelea kuiweka nchi hiyo katika hatari ya mashambulio. Lakinim bali na hilo.
Pia baadhi wanahisi wakimbizi hao ndio wa kulaumiwa kwa kupanda gharama ya makaazi hasa katika maeneo ya Nairobi kama vile Eastleigh, wanakoishi kwa wingi zaidi.