WASHITAKIWA wawili wa wizi wa vifaa vya minara ya simu vyenye thamani
ya zaidi ya Sh milioni 26, mali ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL)
wamehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Sumbawanga mkoani
Rukwa, kutumikia kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja.
Pia, mahakama hiyo imeamuru kila mmoja acharazwe viboko 15 kwenye makalio mara tu watakapoanza kutumikia adhabu hiyo.
Mahakama hiyo pia imeamuru washtakiwa hao kulipa Serikali kupitia
TTCL Sh milioni 26.05, mara tu watakapomaliza kifungo chao, kiasi
ambacho kinalingana na thamani ya fedha ya mali waliyoiba.
Hata hivyo, washitakiwa hao, Emanuel Usambo (27) na David Emanuel
(32), hawakuwepo mahakamani hapo wakati Hakimu wa Mahakama hiyo , Adam
Mwanjokolo alipokuwa akisoma hukumu hiyo kwa kuwa walikuwa wameruka
dhamana.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mwanjokolo aliamuru washitakiwa hao
wasakwe popote walipo na kukamatwa, huku akisema Mahakama hiyo
imeridhika na pasipo shaka yoyote na ushahidi uliotolewa na upande wa
mashitaka ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi , Thomas
Kilakoi kuwa washakiwa hao walitenda kosa hilo .
Upande huo wa mashtaka uliita mahakamani hapo mashahidi watano ambapo washtakiwa hawakuweza kuita shahidi yeyote .
Mwanjokolo alisema kuwa amelazimika kutoa adhabu hiyo kali kwa
washtakiwa hao ili iwe fundisho si kwao tu bali pia kwa wale wote wenye
tabia kama hiyo .
Awali, Mwendesha Mashtaka , Kilakoi iliieleza Mahakama hiyo kuwa
washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo , Januari 23 mwaka huu,
usiku , kijijini Mkima wilayani Sumbawanga ambapo walibomoa stoo mali ya
TTCL na kuiba betri nane za solar zenye thamani ya Sh milioni 24 na
vipande vya nyaya zake tisa zenye thamani ya Sh 2,050,000.