WATU 16, wakiwamo watoto 13 wenye umri chini ya miaka mitano,
wamekufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa
Tanganyika.
Ajali hiyo inayoelezwa kusababishwa na upepo mkali ziwani, ilitokea
jana kati ya Kijiji cha Kipwa na Bandari ya Kasanga kwenye mwambao wa
Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya
Kalambo, Dk Hosea Mang’ombe, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Dk Mang’ombe alifanunua kuwa watoto hao ni miongoni mwa wakazi wa
Kijiji cha Kipwa, waliopelekwa katika Kijiji cha Kapele wakiwa na mama
zao kupewa chanjo, na baadhi yao walikuwa wamekwenda kliniki.
Kwa mujibu wa Dk Mang’ombe, miili ya watoto 13 na akinamama wawili
iliopolewa jana huku mwili wa mjamzito ukiwa haujapatikana hadi jana.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo kwa masharti ya kutoandikwa majina
yao gazetini, walidai kuwapo uwezekano wa kuongezeka kwa idadi ya
waliokufa.
“Idadi ambayo haijafahamika ya wanawake baadhi yao wakiwa wajawazito,
walikuwa na watoto hao wenye umri wa chini ya miaka mitano kwenda
Kapele kupata huduma ya afya…baadhi walikuwa wakihudhuria kliniki,”
alisema mtoa habari huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema
uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali
uliovuma katika ziwa hilo, baada ya boti kufika kati ya Kijiji cha Kipwa
na Bandari ya Kasanga. Hata hivyo, alisema hadi jana majina ya marehemu
hayajapatikana.
“Taarifa kamili nitawapa kadri nitakavyokuwa nikizipata kwa kuwa
haijafahamika idadi kamili ya abiria waliokuwa wakisafiri katika mtumbwi
huo,” alisema Kamanda Mwaruanda.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, uchunguzi wa ajali hiyo na juhudi za
kuopoa miili bado zinaendelea kwa ushirikiano wa wananchi na viongozi
wa vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika.
|