Wachezaji wa Yanga na Azam wakitoshana Nguvu Uwanjani |
Dar es Salaam. Vita ya Klabu ya Yanga na Azam TV
imechukua taswira mpya baada ya Serikali kuziagiza pande hizo kukutana
na kufanya mazungumzo ili kumaliza tatizo kati yao.
Yanga ndiyo klabu pekee ya Ligi Kuu kati ya 14,
iliyosusa udhamini wa Azam TV, ambayo imeingia mkataba wa kuonyesha
mechi za Ligi Kuu kwa kutoa kiasi cha Sh100 milioni kwa mwaka kwa kila
klabu.
Uongozi wa Yanga haukuridhishwa na udhamini huo
ikidai, pamoja na sababu nyingine, kiasi cha pesa kilichopangwa kutolewa
na Azam ni kidogo kulinganisha na udhamini waliopata kutoka Kampuni ya
Pepsi. Kufuatia hali hiyo, Yanga ilikwenda kulalamika serikalini, ambapo
pande husika Yanga, viongozi wa Bodi ya Ligi, wawakilishi wa Azam na
viongozi wa TFF zilikutana na kwa lengo la kutafuta suluhisho.
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Fenella
Mukangara aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alikubaliana na hoja
zilizowasilishwa pande zote mbili, lakini akaagiza zikutane na kufikia
mwafaka.
“Abubakar Bakharessa (mwakilishi wa Azam)
amekubali kukaa mezani na Yanga kuzungumzia masilahi ya pande zote mbili
na Yanga watapewa mkataba waangalie na kama watakuwa na hoja zao za
msingi zitaingizwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Wallace Karia
aliliambia gazeti hili jana kuwa, serikali imeagiza Yanga na Azam kukaa
meza moja kabla ya kusaini mkataba wa udhamini.
“Tumefikia mwafaka. Suala hili sasa limebaki kwa
Yanga na Azam wenyewe kumalizana. Tunamshukuru Waziri Mukangara kwani
hakuna lililoharibika,” alisema Karia.
Habari ambazo gazeti hili limezipata baadaye,
zimesema kuwa Azam na Yanga wanatarajia kukutana leo kujadili
kilichoagizwa kwenye kikao cha jana.
“Azam wako tayari kuzungumza na Yanga, na wamesema
hawana tatizo, lakini ikitokea wakashindwa kuelewana, basi Yanga
watakuwa na uamuzi wao binafsi,” alisema mtoa habari ambaye hakutaka
jina lake kuandikwa kwenye gazeti kwa vile siyo msemaji.
Yanga ilipeleka malalamiko kwa Waziri Mukangara ya
kugomea udhamini wa Azam TV kwa kile walichodai kulazimishwa ikubali
mkataba huo.Uongozi wa klabu hiyo ulisema hauna tatizo na uamuzi wa
klabu zingine kukubali udhamini wa Azam, ila kupinga kwao ilikuwa kwa
lengo la kutaka kushirikishwa kikamilifu.