PONDA ASOMEWA MASHTAKA AKIWA WODINI

Habari zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa, ilikuwa Sheikh Ponda aondolewe hospitalini hapo na kwenda jela, lakini Wakili Nassor alisema hali ya mteja wake haikuwa nzuri tangu asubuhi hivyo kuomba abaki hospitalini hapo. 
Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesomewa mashtaka ya uchochezi akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi).

Ponda aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi tangu Agosti 9 mwaka huu, alipofikishwa hospitalini hapo kwa matibabu, alisomewa mashtaka hayo na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa.

Kiongozi huyo alifikishwa hospitalini hapo baada ya kudaiwa kupigwa risasi ambayo hata hivyo, si Moi wala Polisi waliothibitisha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, ililazimika kuhamia hospitalini hapo kutokana na Ponda kulazwa.

Mwendesha Mashtaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka alisema Sheikh Ponda anatuhumiwa kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sheikh Ponda alikana shtaka hilo bila kuwapo wakili wake, Juma Nassor. Hivi sasa kiongozi huyo wa Kiislamu, anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja kutokana na kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili.

Habari zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa, ilikuwa Sheikh Ponda aondolewe hospitalini hapo na kwenda jela, lakini Wakili Nassor alisema hali ya mteja wake haikuwa nzuri tangu asubuhi hivyo kuomba abaki hospitalini hapo.

“Hawezi kuondolewa kwa kuwa tangu asubuhi analalamika kuumwa kichwa, kizunguzungu na maumivu katika jeraha alilopata. Zaidi ya yote, ni mpaka atakapopata ruhusa ya daktari,” alisema wakili huyo.

Habari zaidi zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa utaratibu unafanyika ili Sheikh Ponda apate ruhusa ya kutoka hospitalini hapo ndipo apelekwe gerezani hadi kesi yake itakapotajwa tena Agosti 28, mwaka huu.

Akizungumza baadaye jana, Wakili wa Ponda alisema: “Nilichelewa kufika, ningepinga mashtaka hayo lakini ninaandaa pingamizi nitakalowasilisha siku ya kutajwa kwa kesi; sikubaliani na mashtaka aliyosomewa mteja wangu na pia Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kusikiliza shtaka linalotajwa.”

Wafuasi wazua zogo
Mapema ilipofika saa 10 jioni, wafuasi wa Sheikh Ponda walifika kwa wingi hospitali kumwona ikiwa ni muda wa kawaida wa kuona wagonjwa, lakini walizuiwa na polisi hali iliyosababisha kutokea kutokuelewana.





 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family