Na Imelda Mtema MSANII wa filamu za Kibongo, Mohammed Mfaume ‘Gado Balloteli’ hivi karibuni alivunjika miguu yake baada ya kuruka kutoka ghorofa ya pili hadi chini wakati akimuonesha msanii mwenzake jinsi ya kuruka. Tukio hilo lilitokea maeneo ya Mwananyamala jijini Dar na kushuhudiwa na wasanii wengine. Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa wasanii hao, Joseph Mteme ‘Baga’ ambaye ndiye aliyekuwa akioneshwa jinsi ya kuruka alisema tukio hilo limetokea wakati wakirekodi Filamu ya Escape. “Nilikuwa najishauri jinsi ya kuruka ndipo Balloteli aliponiambia anioneshe ninavyotakiwa kuruka, ghafla alianguka vibaya na kuvunjika miguu,” alisema Baga kwa majonzi. Baga alisema baada ya tukio hilo shughuli ya kurekodi filamu hiyo ilisimama na kila mtu akakimbilia kumuangalia mwenzao huyo. “Baada ya kufika chini tulimkuta Balloteli akiwa katika hali mbaya, tukamkimbiza Hospitali ya Mwananyamala ambapo iligundulika kwamba amevunjika miguu na kuwaacha wasanii wengine kama King Majuto (Amri Athuman), Kupa (Idrisa Makupa), Hemed (Suleiman) wakiwa katika mshangao mkubwa,” alisema Baga. GPL |