Takwimu
zinaonyesha mabadiliko ya idadi ya wakazi vijijini kwenda mijini ni
kubwa. Katika nchi ya Tanzania idadi ya watu waishio mjini wataipiku
idadi ya watu waishio vijijini ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia
upatikanaji wa miundombinu ni hafifu kwa sekta zote, na hivyo ni vigumu
kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya watu.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi
zinazoendelea, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo
ya miji zikiwemo; ongezeko la watu kwa kasi mijini; miundombinu
isiyokidhi mahitaji ya uendeshaji wa miji; uwezo mdogo wa rasilimali kwa
ajili ya kutoa huduma toshelevu za jamii na kupanuka kwa kasi kwa
maeneo ya miji bila kuzingatia taratibu za Mipango miji na Usimamizi
usiokidhi kasi ya maendeleo ya miji katika Halmashauri zetu
Hata hivyo jitihada zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania katika
miradi mbalimbali zitaleta ahueni ya tatizo linalofikiriwa kutokea, ikiwa ni
pamoja na miradi ya TSCP, Mpango wa Kuimarisha
Serikali za Mitaa Mijini (ULGSP) na hata mradi unaofanana na TSCP na ULGSP,
mahususi kwa Jiji la Dar es Salaam, (Dar es Salaam
Metropolitan Development Project - DMDP), ulio katika mchakato wa kujiandaa kwa utekelezaji wake.
Mradi wa
uendelezaji Miji (TSCP) unaoendelea kutekelezwa katika Miji 7 nchini (Arusha,
Dodoma,Tanga, Mbeya, Mwanza, Mtwara na Kigoma), umezaa matunda kwa mradi
mwingine wa ULGSP. Hali hii ilielezwa rasmi na Waziri Mkuu, Mizengo K. Pinda
(Mb.) wakati akizindua mradi huo wa ULGSP – 18 juni, Kuringe Hall – Moshi.
Akitoa
pongezi zake kwa timu ya TSCP, alisema kuwa mafanikio yaliyoonekana katika
mradi wa TSCP yamerahisisha kupatikana kwa mkopo mwingine kutoka Banki ya Dunia
kwa ajili ya kuendeleza azma hiyo hiyo, mradi huo umejikita katika kuimarisha
Halmashauri za Miji 18, ambazo ni Miji yote iliyobaki ya Tanzania Bara, na
mradi utagharimu kiasi cha Dola milioni 255 kwa kipindi cha miaka mitano.
Aidha Mhe.
Pinda alieleza kuwa jambo muhimu sana la kuzingatiwa na kuhakikisha kuwa mradi
huu unatekelezwa kwa kiasi cha watu kujidhihirishia wenyewe kwa kuona kwa
vitendo mafanikio, alieleza kuwa Serikali haitafumbia macho uzembe au
ubadhirifu wa fedha au vifaa utakaosababisha kazi hii kukwama au kutekelezwa
chini ya kiwango.
Pia Mhe.Pinda
alisisitizia Wananchi kushirikishwa kikamilifu, alisema; “Nasisitiza wadau wote washirikishwe katika ngazi zote na taarifa za
utekelezaji wa mradi ziwekwe wazi ili wadau wote wajue, watoe maon ya kukosoa
au kuboresha”. Aliendelea kusema; “Kwa wale wanasiasa wenzangu, ni fursa ya
kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mradi unafanikiwa kama tunavyotarajia”.
Aidha
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Philippe Dongier alieleza furaha
yake ya kuona maendeleo mazuri ya utekelezaji wa TSCP, na kueleza kuwa ana
matarajio makubwa zaidi na ULGSP. Alisema; “Lengo kuu la Mpango ni kujenga na kuimarisha uwezo
wa Halmashauri kutoa huduma na usimamizi wa Miji. Kupitia mpango huu, mabadiliko ya ufanisi ya
muda mrefu yanatarajiwa katika maeneo ya Mipango Miji, mfumo wa kudhibiti
fedha, uwajibikaji, uendeshaji na matengenezo na ukusanyaji wa mapato”.
Miji
husika (18), imeshaandaa Mipango Mikakati tayari kwa kuanza utekelezaji ifikapo
mwezi Julai 2013.Mradi umelenga kuendelea kuziimarisha
Halmashauri za Miji katika maeneo makuu matano ili ziweze kutoa huduma bora
zaidi kwa kuzingatia sera ya Ugatuaji Madaraka (D by D).
Maeneo yaliyolengwa ni pamoja na; Uboreshaji wa mfumo wa
Mipango miji, ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan mapato yatokanayo na kodi ya
majengo, uboreshaji wa mifumo ya udhibiti wa fedha, manunuzi na masuala ya
mazingira na kijamii, uboreshaji wa mifumo ya utekelezaji, uendeshaji na
utunzaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za jamii, na kuboresha uwajibikaji
na uwazi. Na baadhi ya shughuli husika zitahusisha; ujenzi wa barabara, masoko,
maeneo ya kupumzika na kudhibiti taka ngumu.
ULGSP ni mradi wa kwanza katika Bara la Afrika
chini ya “Mpango kwa Matokeo” (Program for Results – P for R). “Mpango kwa
Matokeo” ni mbinu ya utoaji fedha kulingana na matokeo ya utekelezaji malengo
mliyojipangia. Chini ya Mpango huu,
Halmashauri husika zitafanyiwa tathmini ya utekelezaji wa vigezo vilivyopangwa
kila mwaka na fedha zitatolewa baada ya matokeo kuhakikiwa.
Mbali na mradi wa TSCP na
ULGSP, Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Benki ya Dunia
na Wadau wengine kuanzia miaka ya 1990 imetekeleza Miradi ya Ukarabati wa
Miundombinu Mijini [Urban Sector
Rehabilitation Project (USRP)]
kuanzia 1997 hadi 2004 kwa gharama ya dola
za Kimarekani million 104.9. Mradi huu ulitekelezwa katika miji 9 ya Tanga,
Moshi, Arusha, Mwanza, Tabora, Morogoro, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam na
Mradi wa kuzisaidia Serikali za Mitaa zote (Local
Government Support Project - LGSP)
kuanzia 2004 hadi 2012 nao ulikuwa ni mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za Kimarekani million 52.