Ugonjwa wa kimeta umelipuka katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mifugo kadhaa. Kutokana
na hali hiyo, wakazi 386 katika kijiji cha Kibaoni kata ya Nanjara Reha
wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa chanjo kufuatia ugonjwa
huo.
Akizungumza
na NIPASHE, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo,
Judathadeus Mboya, alisema Aprili 5, mwaka huu katika Kata ya Nanjara
Reha ng’ombe mmoja wa Afisa Mtendaji wa kata ya Ubetu Kahe, Peter
Kavishe, aliugua na baada ya kuzidiwa mmiliki wake aliichinja na kuiuza
nyama kwa bei nafuu katika kijiwe kwa Mafungu.
Mboye alisema Aprili 15 mwaka huu, Ofisa huyo ambaye aliugua na
alizidiwa kutokana na ugonjwa wa kutokewa na malengelenge makubwa meusi
na kukimbizwa katika hospitali ya Huruma. Mboya alisema usiku wa
kuamkia Aprili 17, mwaka huu Kavishe alifariki dunia.
Mkurugenzi huyo lifafanua kuwa uongozi wa hospitali hiyo alipokuwa
amelazwa Kavishe, baada ya kuchukuwa vipimo walishindwa kuvibaini kwa
haraka na kuvipeleka katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kubaini kuwa
ni ugonjwa wa kimeta.
“Siku hiyo ya tarehe 17, mgonjwa mwingine ambaye alikula nyama hiyo
alilazwa katika hospitali ya Huruma na bado anaendelea na matibabu,”
alisema Mboya na kuongeza:
“Halmashauri imejitahidi kutoa chanjo kwa watu waliokula nyama na
kufikia Aprili 20, mwaka huu watu waliopatiwa chanjo wamefikia 386.”
Hata hivyo, Mboya alisema hadi kufikia juzi idadi rasmi ya mifugo waliokufa kutokana na ugonjwa huo haikujulikana.
Naye Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Rombo, Frank Mwanri, alimtaja bakteria
ambaye huambukia ugonjwa huo kuwa ni Basilus anthrax na dalili za
ugonjwa huo ni mifugo kutoa damu isiyoganda katika maeneo yote yenye
uwazi. Mwanri aliongeza kuwa pia kimeta huenea kwa njia ya damu kwa
kushika damu au nyama ya mfugo ambao tayari umeathirika na ugonjwa huo.
Alisema chanjo kwa ajili ya mifugo ilitarajiwa kuanza rasmi jana
wilayani humo.
“Wananchi wote wilayani Rombo, chanjo itaanza rasmi kesho (jana), hivyo
tujitokeze kwa wingi ili kupata chanjo ya ugonjwa huu na kuepusha
madhara ambayo yanaweza kujitokeza na hata maafa kama tusipoangalia,”
alisema Mwanri.
CHANZO: NIPASHE