UBINGWA wa Manchester United jana umeifanya klabu hiyo iweke rekodi nyingine.
Taji hilo linakuwa la 13 kwa Sir Alex
Ferguson katika misimu 21, lakini United pia sasa inakuwa klabu yenye
mafanikio zaidi katika soka ya England kihistoria kwa kutwaa mataji 20.
Kutoka taji lao la kwanza mwaka 1908,
hadi kikosi cha maajabu cha 'Busby Babes' miaka ya 1950, 'Holy Trinity'
miaka ya 1960 na mafanikio ya Ferguson kwa miaka 20 iliyopita, mashabiki
wa United wana mengi ya kutazama nyuma juu ya makali ya timu yao.
Katika picha hizi maalum, BIN ZUBEIRY kwa msaada wa Sportsmail inakuletea picha moja moja kutoka kila enzi za mafanikio ya Mashetani Wekundu.
1907-08: MANGNALL NA MEREDITH WAIWEZESHA UNITED KUTWAA TAJI LA KWANZA
Kikosi kilichotwaa taji la kwanza mwaka
1908. Ernest Mangnall (kulia kabisa) aliiongoza United katika mafanikio
hayona ni sahihi kwamba Mangnall, Sir Matt Busby na Sir Alex Ferguson tu
ndio wameipa mataji United. Sandy Turnbull (aliyekaa katikati chini, wa
tatu kutoka kulia) alifunga mabao 25 katika mechi 30, wakati
mshambuliaji Billy Meredith (aliyekaa kushoto kabisa) alikuwa mmoja wa
nyota wakubwa wa timu. United ilishinda mechi 13 kati ya 14 za mwanzo
ikimaliza msimu inaizidi kwa pointi tisa Aston VIlla. Ni sahihi
kufikiria huu ulikuwa mwanzo wa mafanikio ya United na sasa Mashetani
hao Wekundu wana mataji 20 ndani ya miaka 105.
1910-11: UNITED YAWAPIKU VILLA KUTWAA TAJI LA PILI NDANI YA MISIMU MINNE
Kikosi cha Manchester United kilichotwaa
taji la pili 1910-11 kikiipiku Aston Villa. Ushindi wa 4-2 dhidi ya
Villa katika mchezo mkali na kuwafanya waingie katika mechi ya kuwania
taji dhidi ya Sunderland, ambayo pia walishinda 5-1, huku Harold Halse
(wa pili kushoto nyuma) akifunga mabao mawili.
1951-52: BUSBY AMALIZA KIU YA MUDA MREFU YA MATAJI UNITED
Mashabiki wa United walilazimika
kusubiri kwa muda mrefu tangu watwae taji la mwisho, walipomaliza
kileleni. Arsenal na Tottenham wote walikuwa wapinzani wa United kwenye
mbio za ubingwa msimu huo, na ushindi wa mechi mbili dhidi ya The
Gunners ulimaliza kazi ngumu ya timu ya Sir Matt Busby. Ushindi wa 6-1
dhidi ya Arsenal katika siku ya mwisho ya msimu uliipa taji United. Hii
ni picha ya Jack Rowley Uwanja wa Preston msimu huo - Rowley ni mmoja wa
wafungaji wa kihistoria Man United, na alikuwa katika kiwango cha juu
msimu huo, akifunga mabao 30 katika mechi 40 za ligi.
1955-56: KIKOSI CHA BUSBY CHAENDELEZA FURAHA YA MATAJI
Kikosi cha makinda kilichoongozwa na Sir
Matt Busby kieliendelea heshim msimu huo. United ilimaliza msimu
ikiwazidi pointi 11 Blackpool na Wolves na kutwaa taji la pili miaka
1950. United ilikuwa inacheza soka maridadi ya kuvutia kwa kushambilia,
na ilifahamika ulimwengu mzima kama 'Busby Babes'. Miongoni mwa nyota wa
msimu huo ni Duncan Edwards na Eddie Colman, na mshambuliaji Tommy
Taylor. Picha hii inamuonyesha Taylor (kushoto kabisa) akifunga bao lake
la pili na la tatu kwa United katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Chelsea
Uwanja wa Old Trafford. Taylor alimaliza msimu na mabao 25 katika ligi.
1956-57: UNITED YATWAA MFULULIZO MATAJI MAKINDA YA BUSBY YAKIENDELEA KUNG'ARA TENA
United ilitwaa mfululizo mataji 1956-57,
kitu ambacho hawakufanya tena hadi mwishoni mwa miaka ya 1990. Sir
Bobby Charlton akiwa kivutio katika kikosi cha Sir Matt Busby msimu huu,
kikiundwa na wachezaji makinda kama Duncan Edwards na Tommy Taylor
walioisaidia United kutwaa taji. Waliwazidi kwa pointi nane Tottenham na
Preston. Ushindi wa 4-0 dhidi ya Sunderland Uwanja wa Old Trafford
ulikamilisha mpango mzika kwa United - hii ni picha ya juhudi za Billy
Whelan akifunga kwa kichwa. Mkali Whelan alifunga mabao mawili siku
hiyo, huku Edwards na Taylor wakifunga mengine. Whelan, Edwards na
Taylor walikuwa miongoni mwa wachezaji wa United waliofariki kwenye
ajali ya ndege ya Munich Air mwaka 1958, janga ambalo lilizimisha kikosi
cha makinda cha Busby.
1964-65: UNITED YAIPIKU LEEDS KUTWAA TAJI LA KWANZA MIAKA YA SITINI
Taji la kwanza kati ya mawili ya miaka
ya 1960 United lilipatikana msimu wa 1964-65, Wekundu hao wakiwapiku
Leeds kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Huku winga kinda
George Best akianza kujijengea jina, na Denis Law akisimama mbele ya
lango la adui, United iliwapiku wapinzani wao wa Yorkshire. Ushindi wa
mbinde wa 1-0 Uwanja wa Elland Road, Aprili, lililofungwa na John
Connelly, uliweka mambo sawa. United ilitwaa taji baada ya kuwafunga 3-1
Arsenal Uwanja wa Old Trafford, siku ambayo Leeds ilitoka sare na
Birmingham. Hii ni picha ya Law akifunga bao la pili, na la tatu kwa
United dhidi ya Gunners.
1966-67: 'HOLY TRINITY' ALIPOIWEZESHA UNITED KUTWAA TAJI TENA
Sir Matt Busby aliiongoza United kutwaa
taji la pili ndani ya misimu mitatu 1966-67, Wekundu hao wakiwazidi kwa
pointi nne Nottingham Forest na Tottenham. Magwiji wa klabu, 'Holy
Trinity' akina George Best, Denis Law na Sir Bobby Charlton walikuwa
kila kitu katika mafanikio haya na United wakawa mabingwa kwa mara ya
saba. Law alifunga mabao 23 kwa United msimu huo na Mscotland huyo
alifunga mabao mawili wakati United ikiitandika West Ham 6-1 Uwanja wa
Upton Park.
1992-93: FERGIE ALIPOMALIZA UKAME WA MATAJI WA MIAKA 26 NA KUANZA KULUNDIKA 'NDOO' O.T.
Wekundu hao walipitia kipindi kigumu cha
miaka 26 bila taji la Ligi Kuu. Kocha wa United, Sir Alex Ferguson
akawasajili Eric Cantona kutoka Leeds katikati ya msimu, katika usajili
ambao utaendelea kuwa kihistoria katika soka ya England. United, Villa
na Norwich zilikuwa katika mbio kali za taji. Ushindi dhidi ya Norwich
Aprili ulifuatiwa na ushindi dhidi ya Sheffield Wednesday Uwanja wa Old
Trafford. United ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 hadi dakika za lala salama,
lakini ikatoka nyuma na kushinda 2-1, shukrani kwake Steve Bruce
mfungaji wa mabao hayo. Hapa, Bruce akishangilia bao lake la ushindi
alilofunga dakika ya 97.
1993-94: TAJI LINGINE KWA MASHETANI WEKUNDU ROBSON AKIRISHA MBAYA...
Eric Cantona, Andrei Kanchelskis, Ryan
Giggs na Mark Hughes waliifanya timu ya Ferguson itishe wakati huo.
United waliporomoka kidogo, lakini ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu, Man
City uliwarejesha barabarani na Wekundu hao wakashinda mechi zao tano
za mwisho msimu huo. Mmoja wa washambuliaji waliokuwa kwenye kikosi cha
United ni Bryan Robson aliyefanya mambo makubwa kwa ujumla miaka ya
1980. Hapa anainua taji na Steve Bruce mwishoni mwa miaka yake 13 katika
timu hiyo.
1995-96: FERGIE AMBWAGA KEEGAN UNITED IKITWAA TAJI LA 10
Alan Hansen alitoa msemo maarufu: "Huna
lolote na watoto' wakati makinda wa United wanafungwa na Aston Villa
katika mechi ya ufunguzi msimu wa 1995-96. United ilikuwa inazidiwa
pointi 12 na kikosi cha Kevin Keegan cha Newcastle mwishoni mwa January.
Newcastle wakapoteza makali na United wakasimama imara. Picha hii
inamuonyesha 'mchawi wa Kifaransa', Eric Cantona akiwafungia wenyeji bao
pekee katika ushindi wa 1-0. Cantona na kipa goalkeeper Peter
Schmeichel walikuwa katika kiwango cha juu katika miezi ya mwishoni ya
msimu huo. Keegan alizodolewa kwa kauli zake dhidi ya Ferguson na United
ikatwaa taji la 10 la ligi kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Middlesbrough
katika siku ya mwisho.
1996-97: TAJI LA NNE NDANI MISIMU MITANO, MWANZO WA UTAWALA WA MAN UNITED NA FERGIE
Makinda wa United wakazidi kukomaa na
kujiamini kutoka kushinda mfululizo na Mashetani Wekundu wakatetea taji
msimu wa 1996-97. Kikosi cha Ferguson kiliwazidi kwa pionti saba wote
Arsenal na Newcastle. Ushindi wa ubingwa ukija mwishoni mwa msimu dhidi
ya Liverpool, huku Gary Pallister akifunga mabao mawili na Andy Cole
moja United wakiua 3-1. Picha hii inamuonyesha Sir Alex Ferguson
akishangilia ushindi Uwanja wa Anfield na Msaidizi wake, Brian Kidd.
Taji hilo la nne katika misimu mitano ulikuwa mwanzo wa United kutawala
soka ya England.
1998-99: MSIMU MZURI ZAIDI WA MATAJI MATATU KWA MASHETANI WEKUNDU...
Kama kuna msimu babu kubwa kabisa kwa
klabu yoyote England, utakuwa wa Manchester United 1998-99 walipotwaa
mataji matatu. United ilikuwa inakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa
kikosi cha Arsene Wenger, Arsenal, lakini kufungwa kwa The Gunners na
Leeds kuliwaachia mwanya United. Wekundu hao walitoa sare na Blackburn
na kisha wakatoa nyuma na kuifunga Tottenham katika siku ya mwisho ya
msimu. Hapa Andy Cole akifunga bao la ubingwa.
1999-2000: UNITED YABEBA TAJI ILE KIBABE HASWA HASWA KWA POINTI 18 ZAIDI
United kubeba taji kibabe haswa chini ya
Ferguson ilikuwa ni 1999-2000, walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa
pointi 18 zaidi. Wakichagizwa na mafanikio ya mataji matatu 1999, United
walikuwa moto. Wasiwasi ulikuja tu pale Wekundu hao walipotolewa katika
Klabu Bingwa nchini Brazil. Wakati hayo yakitokea, wapinzani wao wote
wakapoteza pointi nyumbani wakati wachezaji wa United wakilaumiana
wenyewe. Mechi yao ya kwanza ya ligi kucheza waliporejea nyumbani
ilikuwa dhidi ya wapinzani wao wa karibu, Arsenal - Teddy Sheringham
(pichani) akishangilia bao lake la kusawazisha na Dwight Yorke, katika
mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1.
2000-2001: HAKUNA WA KUIZUIA UNITED WEKUNDU HAO WAKITWAA TAJI LA TATU MFULULIZO
United walitwaa tena taji la Ligi Kuu
2000/2001 - wakiizidi kwa pointi 10 Arsenal, licha ya kupoteza mechi zao
tatu za mwisho msimu huo. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika historia
ya United kutwaa mara tatu mfululizo ubingwa wa ligi. Ushindi wa 6-1
dhidi ya Arsenal Februari, siku ambayo Dwight Yorke alifunga mabao
matatu, kilikuwa ni kitu cha kukumbukwa msimu huo. Hapa kikosi cha
United kikisherehekea ubingwa wa saba wa Ligi Kuu katika miaka tisa,
ambao ulidhihirisha umwamba wao England.
2002-03: MASHETANI WEKUNDU WAIDUWAZA ARSENAL WAKITOKA NYUMA NA KUTWAA UBINGWA
Arsenal iliiacha kwa pointi nane United
ikiwa imebaki miezi mitatu msimu wa 2002-03, lakini United walizinduka
na kupambana hadi kuwapiku The Gunners. Wekundu hao walicheza soka ya
kuvutia mwishoni mwa msimu huo, na utamu zaidi ulikuwa pale
walipoitandika Newcastle 6-2 Aprili. Hii ni picha ya Paul Scholes
akifunga bao lake la kwanza kati ya matatu kwa United katika mechi hiyo.
Sare ya 2-2 na Arsenal katika mechi iliyofuata iliwafanya United
walingane kwa pointi na The Gunners na hatimaye Ferguson akasherehekea
ubingwa mwishoni baada ya Arsenal kupoteza pointi mbele ya Bolton na
United ikitwaa taji la 15.
2006-07: UNITED YAREJEA MATAWI YA JUU FERGUSON AKIMGARAGAZA MOURINHO
United ilihitaji sana taji la Ligi Kuu
msimu wa 2006-07, baada ya kulikosa kwa misimu mitatu. Jose Mourinho wa
Chelsea alikuwa ametwaa mataji mawili yaliyopita na walikuwa wapinzani
kweli. Mchuano ulikuwa mkali na wakati wote walizidiana kwa pointi
chache. Katika moja ya mechi ngumu ilikuwa Uwanja wa Goodison Park,
United walipotoka nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Everton na kushinda 4-2.
Hii ni picha Wayne Rooney akishangilia baada ya kuifungia United bao la
nne. Wikiendi iliyofuata, United iliwafunga jirani zao, Manchester City,
na Chelsea ikatoa sare na Arsenal, hivyo Wekundu hao kubeba taji.
2007-08: MKALI GIGGS ATIKISA NYAVU UNITED WAKIENDELEZA UTAWALA
Ulikuwa msimu mwingine wa miujiza,
United wakitwaa taji siku ya mwisho kwa mara ya kwanza ndani ya miaka
tisa. Kikosi imara cha Arsenal kilikuwa mbele kwenye mbio za ubingwa
2008, lakini United ikawatoa barabarani. Mwishoni mwa msimu, Chelsea
nayo ikakamata barabara, ikiwafunga Man United Uwanja wa Stamford Bridge
na kuwafikia kwa pointi zikiwa zimebaki mechi mbili. United, ikiwa na
wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ilihitaji kushinda mechi
zake mbili zilizobaki. Waliifunga West Ham Uwanja wa Old Trafford na
baadaye Wigan 2-0 katika siku ya mwisho. Pichani Ryan Giggs akifunga bao
gumu la pili, katika siku ambayo alifikia rekodi ya Sir Bobby Charlton
kucheza mechi 758 United. Sir Alex Ferguson, ambaye aliserebuka katika
mvua uwanjani, alitwaa taji la 10. Akiwa na damu changa za akina
Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Carlos Tevez kikosini, United pia
ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa msimu huo.
2008-09: WAPINZANI WAKUU, LIVERPOOL WAPIGWA UNITED IKITWAA TAJI LA 18
Msimu wa 2008-09 mbio za ubingwa
zilikuwa shughuli pevu, huku Liverpool ikiwa katika nafasi nzuri
kileleni na United walilazimika kutokea chini kuwapiku. Lakini moto
waliorudi nao mwaka mpya vijana wa Ferguson uliwawezesha kubadilisha
sura ya ligi. Federico Macheda, kinda wa miaka 17 wakati huo aliyekuwa
hajulikani na yeyote Old Trafford alitokea benchi na kufunga bao la
ushindi dhidi ya Aston Villa, United ikishinda 3-2 na kuwaengua
kileleni Liverpool kwa mara nyingine tena. United walitwaa kwa mara
nyingine kwa mara ya tatu mfululizo taji la Ligi Kuu na la 18 jumla,
wakifikia rekodi ya Jogoo la Merseysiders. Ilikuwa furaha kubwa kwa
mashabiki wa United kuona timu yao inafikia rekodi ya kutwaa mara nyingi
ubingwa wa Ligi Kuu ya Liverpool iliyotawala miaka ya 1970 na 1980.
2010-11: REKODI YAVUNJWA, TAJI LA 19 LAWAFANYA UNITED WAWE WAO TU
Wakosoaji wengi walikionda kikosi cha
Manchester United cha 2010-11 kwamba hakikuwa katika ubora wake, lakini
kilimudu kutwaa ubingwa tena, licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa klabu
mbili za London, Arsenal na Chelsea. Ushindi wa 2-1 kwa United dhidi ya
Chelsea Mei ulitosha kuibebesha ubingwa United iliyotoa sare na
Blackburn katika mchezo uliofuata. Hii ni picha bao bora lililofungwa na
Wayne Rooney kwa tika tak lililowapa ushindi United dhidi ya mahasimu
City Uwanja wa Old Trafford. Taji la 19 kwa United lilikuwa ni rekodi
nyingine, wakiipiku Liverpool na kuifanya klabu hiyo kuwa yenye
mafanikio zaidi katika soka ya England.
2012-13: CITY NA MANCINI SI LOLOTE KWA FERGIE AKIIONGOZA UNITED KUBEBA TAJI LA 20
Sir Alex Ferguson na United walipania
kurejesha taji la Ligi Kuu walilolipoteza mbele ya jirani zao,
Manchester City sekunde za mwishoni msimu wa 2011-12. na wamefanikiwa
kutimiza azma hiyo baada ya vita ya miezi. Picha hii inamuonyesha Robin
van Persie akipiga mpira wa adhabu dakika za lala salama uliowapa bao la
ushindi United katika ushindi wa 3-2 dhidi ya City. Van Persie,
aliyesajiliwa kutoka Arsenal msimu huu, ndiye amekuwa chachu ya ubingwa
wa United katika miezi yake sita ya mwanzoni, na bao lake hili la
ushindi katika mechi ya Desemba uliipaisha United kileleni kwa pointi
tano zaidi dhidi ya jirani zao. United iliendeleza moto hadi jana kutwaa
taji la 20.