SERIKALI imetangaza rasmi kuwa maji
yanayofaa kwa matumizi mbalimbali, yanaendelea kupungua mwaka hadi
mwaka, kutokana na ongezeko la watu na shughuli mbalimbali za uzalishaji
wa mali.
Kiasi cha maji kilichopo kwa sasa kwa
kila mtu ni wastani wa lita milioni 2.02 kwa mwaka, lakini inakadiriwa
ifikapo mwaka 2025 kiwango kitapungua kufikia lita milioni 1.5.
Shughuli za uzalishaji umeme, kilimo cha
umwagiliaji, matumizi ya viwandani na majumbani ni chanzo kikubwa cha
upungufu wa maji sanjari na uharibifu wa maeneo oevu.
Aidha, Waziri wa maji Profesa Jumanne
Maghembe amesema katika hotuba yake ya bajeti aliwasilisha bungeni leo,
kuwa kufikia Februari mwaka huu hali ya upatikanaji wa maji haikuwa
nzuri, kutokana na uhaba wa mvua za vuli katika maeneo nchini.
“Kwa ujumla, hali hiyo ilisababisha
kiasi cha maji katika mabwawa, mito na maziwa kupungua ikilinganishwa na
mwaka uliopita,” alisema.
Alisema katika bonde la Ruvuma na Pwani
ya Kusini kiasi cha mvua katika kipindi hicho kilikuwa ni milimeta 550
kwa upande wa Magharibi wa bonde (Songea) na kwa upande wa mashariki wa
bonde (Mtwara) ni milimeta 800 ikilinganishwa na kiasi cha mvua cha
kawaida cha milimeta 1,000.
Katika bonde la mto Pangani hadi Aprili
10 kina cha maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kilikuwa meta 682.53
juu ya usawa wa bahari, kutokana na mvua kunyesha chini ya wastani. Hali
pia ni mbaya katika Bonde la Mto Rufiji, ambako kuna Bwawa la Mtera.
Ziwa Tanganyika nalo limekuwa likipungua
na upatinakaji wa maji katika mto Wami na Ruvu umekuwa ukipungua. Hata
hivyo, alisema katika hotuba yake kuwa bonde pekee ambalo kwa ujumla
wingi wa maji uliongezeka ni ni bonde la Ziwa Victoria.
Alitoa wito kwa Watanzania kuchukua hatua za makusudi za kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuinusuru rasilimali hiyo.
Alisisitiza kuwa jukumu si la serikali
pekee bali ni la wote. Pamoja na kuelezea uhaba wa maji, Waziri Maghembe
alisema kwamba uzalishaji wa majisafi kwa mamlaka zote 19 za miji mikuu
ya mikoa, uliongezeka kutoka wastani wa lita 330.99 kwa siku kufikia
lita milioni 341.77.
Alisema ongezeko hilo, limetokana na
ukarabati wa miundombinu ya maji iliyokamilika na inayoendelea kujengwa
katika miji mikuu ya mikoa mbalimbali.
Waziri Maghembe alisema kutokana na
mabadiliko ya tabianchi imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na hali
hiyo, kama kujengwa mabwawa madogo na makubwa ya kuhifadhi maji,
kuimarisha ukusanyaji wa takwimu zinaozohusu raslimali za maji,
kuelimisha umma ili kuongeza weledi kuhusu mabadiliko na kutumia
utaalamu asilia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema mkakati mwingine wa kukabiliana
na uhaba wa maji ni kuweka muundo bora kitaasisi, kwa ajili ya usimamizi
endelevu wa raslimali za maji, ingawa wanakabiliwa na changamoto la
bajeti ndogo.