VINARA wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, Yanga, leo watakuwa na kibarua kingine kigumu wakati watakapoialika Kagera Sugar ya Missenyi mkoani Kagera kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mechi ambayo ni muhimu kwa timu zote mbili.
Mbali na mechi hiyo, kutakuwa na mechi nyingine nne leo zikihusisha timu za Coastal Union dhidi ya Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Polisi Morogoro dhidi ya Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu dhidi ya Toto Africans (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar dhidi ya Prisons (Manungu).
Macho na masikio ya wapenzi wengi wa soka yatakuwa yanaelekezwa kwenye Uwanja wa Taifa ambako timu hiyo kongwe ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam itakuwa inasaka pointi tatu muhimu ili kujikita zaidi kwenye kilele cha msimamo; katika mechi ambayo viingilio ni vya Sh 5,000 (viti vya bluu na kijani), Sh 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), Sh 15, 000 (VIP C na B) na Sh 20, 000 (VIP A).
Yanga inayonolewa na kocha kutoka Uholanzi, Ernest Brandts, inaongoza ligi ikiwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 17, na ushindi leo utakuwa muhimu hasa ikizingatiwa kuwa inafukuzwa kwa karibu na Azam FC ya Dar es Salaam.
Azam FC ambayo Jumamosi iliyopita ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa vijana hao wa Brandts, wako nafasi ya pili wakiwa na pointi 36, na watakuwa wanaiombea dua mbaya Yanga leo kwani endapo itapoteza mchezo huo au kusimamishwa, itakuwa nafuu kwao.
Lakini ushindi dhidi ya Azam FC, umekuwa ni morali tosha kwa Yanga kuweza kuendeleza wimbi la ushindi na hasa ikifahamu kuwa ushindi leo, utaiacha pointi sita Azam na huku wakifungana kwa michezo.
Ni kutokana na hali hiyo, mechi ya leo inatarajiwa kuwa ya ushindani na hasa ikikumbukwa kuwa Yanga ilitaabika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika mechi ya kwanza na kulala bao 1-0.
Mbali ya hilo, Kagera Sugar itakuwa inawania kujipatia ushindi ili kuendeleza ubabe wake kwa Yanga, lakini pia ikitaka pointi tatu zitakazoiwezesha kusogea mbele katika msimamo na kufungana na Simba yenye pointi 31, huku ikiiombea mabaya Coastal Union.
Timu hiyo ya walima miwa wa Missenyi, ina pointi 28, tatu nyuma ya Simba ambayo haichezi leo, na pointi mbili nyuma ya Coastal Union inayoikaribisha Ruvu Shooting. Inashika nafasi ya tano.
Ushindi kwa Coastal Union utaiwezesha kukaa katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33, tatu nyuma ya Azam FC na pointi mbili mbele ya mabingwa watetezi Simba ambao hawana mechi wiki hii kwani watakuwa safarini kwenda Angola kurudiana na Recreativo de Libolo katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mtibwa Sugar nayo baada ya kuizamisha Simba mwishoni mwa wiki kwa bao 1-0, itakuwa na kazi ya kuendeleza wimbi hilo kwa kuikabili Prisons, huku katika siku za karibuni ikiwa na rekodi ya kutofanya vizuri nyumbani kwake Manungu mjini Turiani.
Kikosi hicho cha nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime, kina nafasi nzuri ya kujisogeza mbele ya msimamo endapo kitashinda mechi hii muhimu, kwani sasa kiko nafasi ya sita, ikiwa ni pointi 27, moja nyuma ya ndugu zao wa Kagera Sugar.
Katika hatua nyingine, mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar, Simba imeingiza shillingi milioni 62