LOWASSA:SERIKALI IKIONGEZA AJIRA,CCM ITASHINDA

ALIYEWAHI kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa amesema Serikali ikitekeleza kwa usahihi maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya suala la ajira, chama kitashinda kiurahisi uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Amesema serikali zote mbili; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar (SMZ) zinapaswa kuzingatia hilo.

Akizungumza katika mahojiano na Radio Uhuru jijini Dar es Salaam, jana juu ya uchaguzi wa Kenya, Lowassa alisema amefurahishwa kuwa suala la tatizo la ajira kwa vijana, limekuwa ni moja ya ajenda muhimu katika uchaguzi huo wa wiki ijayo.

“Nimefurahi kuwa wenzetu wameliona hili kuwa ni tatizo kubwa nan i ajenda muhimu katika uchaguzi wao. Nimefurahi Waziri Mkuu Odinga alielezea jinsi serikali yao ilivyojaribu kulishughulikia suala hili,” alisema Lowassa.

Alisema ni muhimu nchi za Afrika Mashariki kutambua rasmi tatizo hilo. Kwa mujibu wake, CCM kimepiga hatua kubwa ya kukiri kuwepo kwa tatizo hilo la ajira kwa vijana, na kimetoa maelekezo kwa serikali zote mbili kulishughulikia.

“Moja ya maazimio ya mkutano mkuu wa CCM ni juu ya suala la ajira na katika kila halmashauri kuu hivi karibuni, tulilijadili kwa kina tatizo hili, na kwa kweli kama serikali zetu hizi zitatekeleza maelekezo yake, sina shaka yoyote CCM tutashinda kiurahisi 2015,’’ alisema.

Lowassa, ambaye amekuwa msemaji mkuu wa suala la ajira kwa vijana akiliita ni bomu linalosubiri kulipuka, aliongeza kuwa uamuzi wa vikao hivyo yakitekelezwa vizuri utakifanya chama kingie kwenye uchaguzi mkuu kikiwa na majibu sahihi yaliyokwishajibiwa. Aidha alisema kilimo ni moja ya eneo ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hilo.

“Pamoja na kwamba bado naamini kuwa elimu kabla kilimo kwanza, lakini sekta hii nakubaliana kabisa kuwa inaweza kusaidia kukabiliana na tatizo hili,’’ alisema.

Kauli ya Lowassa imekuja siku moja baada ya Shirika la Utafiti la Synovate kutoa matokeo ya uchaguzi wake yanayoonesha kuwa CCM kimeongezeka umaarufu ambapo asilimia 52 ya wananchi waliohojiwa wamesema wangependa kujiunga nacho.

Kwa upande wake Lowassa, utafiti huo umebainisha umaarufu wake kuelekea 2015 umepanda kwa asilimia sita na kufikia asilimia saba akiwa miongoni mwa vigogo watano wa juu wanaopewa nafasi ya kushinda urais iwapo uchaguzi ungefanyika

                    

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family