MTOTO anayekadiriwa kuwa na umri wa siku moja aliyekutwa juzi akiwa ametelekezwa vichakani Kimara Baruti, Manispaa ya Kinondoni, imebainika aliyemtupa alikuwa mfanyakazi wa ndani katika eneo hilo.
Kuna taarifa zinazodai kuwa, msichana aliyedaiwa kufanya kitendo hicho, alikamatwa juzi na polisi kutokana na taarifa za wasamaria waliomshitukia baada ya kumwona hana ujauzito.
Inaelezwa kwamba msichana huyo alikutwa akiwa na hali mbaya kiafya, kutokana na kutokwa na damu nyingi. Kutokana na mtoto huyo mchanga kutupwa eneo jirani na nyumbani anakoishi, msichana huyo alipoona anaweza kugundulika, aliomba aende shambani.
“Kuna watu walikwenda kutoa taarifa polisi. Polisi walimkamata akiwa shamba maeneo ya Bonyokwa. Walikuta akitokwa damu nyingi,” alisema jirani akitaka jina lake lisiandikwe gazetini.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, walimpeleka Hospitali ya Tumbi Kibaha kabla ya kumrudisha kituo kidogo cha polisi cha Mbezi.
Mkazi wa Baruti Bondeni, Mary Mloge, ndiye alimwokota mtoto huyo juzi alfajiri wakati akienda kazini. Mtoto huyo wa kiume inadaiwa kitovu chake kilikuwa kimekatwa lakini bila kufungwa.
Akizungumza na gazeti hili, Mloge alisema alipofika eneo lililo na bonde na miti eneo la Baruti, alisikia sauti ya mtoto akilia. Polisi wa kituo cha Rombo walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Sinza na baadaye Hospitali ya Mwananyamala.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa zaidi za tukio hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi katika ziara ya Rais.