Sakata la mchezaji mkongwe nchini Juma Kaseja na klabu yake ya Yanga
leo limechukua sura mpya, baada ya kudumu kwa takribani miezi kadhaa.
Kaseja ambaye amekuwa kwenye mgogoro wa malipo ya fedha za usajili na
uongozi wa Yanga mpaka akafikia hatua ya kugoma kufanya mazoezi na timu
hiyo wakati wa uongozi wa kocha Marcio Maximo, leo hii klabu ya Yanga
imeamua rasmi kukata mzizi wa fitna na kumuacha mchezaji huyo
waliyemsajili msimu uliopita baada ya kuachwa na Simba. Akizungumza mjini hapa, Mkurugenzi wa Habari wa Yanga, Jerry Muro amesema Kaseja amevunja mkataba kutokana na kutokwenda mazoezini kwa saa 48. “Kaseja haidai Yanga na fedha zake aliishalipwa, tarehe zinaonyesha siku fedha hizo zilipolipwa. “Pia katika mkataba hakukuwa na sehemu inaonyesha ni lazima Kaseja alipwe siku fulani lakini ilikuwa ni lazima alipwe ndani ya kipindi cha mkataba. “Yeye aliamua kususa kuja kazini, jambo ambalo lilivunja mkataba wake na Yanga. “Kwa kuwa hatudai, tumeona ni vema kumuachia aende aendako na tunamtakia kila la kheri kama klabu ya Yanga,” alisema Muro. Muro pia amedai kuwa Kaseja alianza kuwa na kinyongo na Yanga baada ya benchi la ufundi kuanza kumtumia Dida kutokana na kuwa na uwezo zaidi kumzidi kwakuwa katika mechi zilizopita alionekana kushindwa kumudu. |