KITABU MAALUM CHA MAFUNZO YA UDEREVA CHAZINDULIWA



MAMLAKA ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma nchini (VETA), imezindua kitabu maalum kitakachotumika katika kutoa mafunzo kwa madereva nchini kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani na matukio mengine.
Mkuu wa Chuo cha Veta Chang’ombe, Samuel Ng’andu anasema kuwa chuo chake kimeandika kitabu hicho ili kitumiwe na vijana wanaojiunga na mafunzo ya udereva pamoja na wadau wengine wa usafirishaji nchini, ili waweze kujua mambo ya msingi hasa ya kisheria yahusuyo taaluma ya usafirishaji wa abiria na vyombo vyake.
Anasema kitabu hicho kilichozinduliwa jijini Mwanza hivi karibuni na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, kina mada za alama za usalama barabarani, vimiminika sahihi vinavyotumika kwenye vyombo vya moto na taarifa mbalimbali zilizo kwenye tairi la gari.
“Mada zilizowekwa ni zile ambazo bado watumiaji wa magari wanazipuuza wanapokuwa barabarani ama wanapotakiwa kufanya matengenezo madogo madogo kwenye magari yao,” anasema. Anaamini kitabu hicho kinaweza kuwa na mapungufu kwenye baadhi ya sehemu, lakini anatoa mwito kwa watumiaji wasisite kuwapatia mrejesho ili waweze kukifanyia marekebisho zaidi siku zijazo.
“Tumeandika kitabu hiki, kutokana na kuguswa sana na tatizo la ajali zinazoendelea kutokea hapa nchini, kila siku watu wakiwemo wataalamu wa kada tofauti hufariki dunia, sio kwamba wanakwenda na kurudi, hapana hawawezi kurudi, inatia uchungu sana,” anafafanua.
Kitabu hicho chenye rangi ya njano, iking’arishwa na picha za magari na mabasi kwa jarida la juu, na picha inayoonesha majengo ya Chuo cha Veta, Chang’ombe kwa jarida la nyuma, kina jumla ya kurasa 33. Anasema kitabu hicho kimechapishwa na wataalamu wa Veta Chang’ombe kwa kushirikiana na Polisi kupitia kitengo cha uchapishaji ili kiweze kuisaidia jamii kujikomboa kifikira kwa kuondokana na tatizo la ajali, ili siku moja ibaki historia kwa vizazi vijavyo.
Anasema jamii ikizingatia machapisho ya usalama barabarani kwa kuyasoma kwa umakini, na kuyatekeleza kwa vitendo, vita ya ajali za barabarani itakuwa rahisi.
“Sote tutakuwa mashahidi wa kushuhudia ushindi, dhidi ya adui wa taifa hili, ‘ajali za barabarani’,” anasema. Anasema hatua ya Veta kutunga kitabu hicho inaonesha kuwa wafanyakazi wake wameanza kuitikia mwito wa viongozi wao wa kujitoa kuandika vitabu vinavyoendana na taaluma zao.
“Veta inaamini kuwa walimu wanapoandika vitabu vinavyoendana na mitaala ya kufundisha, vitawafanya wahitimu wetu kukubalika kwenye soko la ajira kwa kuajiriwa na kujiajiri wenyewe kwani vitabu hivi huandikwa kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na tafiti mbalimbali,” anaeleza na kuongeza kuwa kitabu hicho kimekamilika kwa usimamizi bora uliofanywa na yeye mwenyewe.
Anasema hatua ya uandishi wa vitabu, imetokana na Veta kujiwekea utaratibu wa kuwapeleka wafanyakazi wake viwandani kupata ujuzi na maarifa mapya juu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa sekta zote, ikiwemo ya udereva.
“Tunawapongeza wafanyakazi wetu , walio tayari kutumia muda wao kuandika vitabu ili taifa letu siku moja liongeze kasi ya maendeleo katika kupambana na ajali,” anasema. Analishukuru Jeshi la Polisi nchini, Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kutoa changamoto mbalimbali ili taasisi zinazoendesha mafunzo ya udereva ziweze kuandika vitabu mbalimbali vya elimu ya udereva.
“Tunaishukuru Kampuni ya BP kwa kuturuhusu kutumia kipeperushi kinachoelezea mojawapo ya kundi la oili kwa gari za kisasa na za zamani na bila ya kumsahau mtungaji wa kitabu cha usalama barabarani kwa makundi ya watu maalum,” anasema na kuwataja walioshirikiana kuandaa kitabu kuwa ni Kisembe Kapele ambaye ni Mkufunzi Mkuu, Mratibu wa Mafunzo Mashaka Kassara, Mkufunzi Msaidizi David Kwegela na Muongozaji Mafunzo ya Udereva, Kigalu Sawaka, wote wakiwa ni kutoka Shule ya Mafunzo ya Udereva ya jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Lwenge aliwashukuru Veta kwa uamuzi wao wa kutunga kitabu hicho, ambacho anasema kitajenga uelewa mpana kwa jamii na hivyo kuifanya nchi kuwa na uwezekano mkubwa wa kuzuia ajali.
“Niwashukuru kwa uamuzi wenu wa kuandika kitabu hiki, ambacho kitakuwa ni dira muhimu kwa watumiaji wetu wa barabara, rai yangu kwa wananchi na madereva naomba watumie sehemu ya muda wao ili waweze kukisoma na kujifunza mambo ya msingi,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Mhandisi Moshi Zebania anasema Veta imetunga kitabu hicho ili kusaidia taifa lijikomboe kifikra katika tatizo sugu la ajali. “Naomba wananchi wakisome kitabu hiki, na tunayo imani kuwa kitakuwa msaada kwa taifa, maana kinafafanua juu ya vimiminika vitumikavyo kwenye magari, magurumu ya magari na mawasiliano wakati dereva anapoendesha gari,” anasema.
Maudhui ya kitabu Kitabu hicho katika ukurasa wake wa kwanza, kinaelezea alama za barabarani, jinsi mtumiaji wa barabara anavyopaswa kutumia alama hizo wakati wa kuendesha gari lake. Mtunzi wa kitabu hicho ambaye katika makala haya atatambuliwa kama Veta kupitia kwa Mkuu wa Chuo cha Chang’ombe, Samuel Ng’andu, anasema mtu hawezi kuwa mchungaji wa kanisa au imamu wa msikiti bila ya kujua Biblia au Quran.
Anaamini kwamba mchungaji au imamu huwaongoza waumini wao kwa kutumia vitabu vya imani zao na sio kwa akili zao. Anasema mtu kujua kuendesha gari kitaalamu ni pamoja na kujua tafsiri sahihi za alama zote, kuzitii na kuziheshimu maana alama ni mwongozo kwa watumia barabara wote nchini.
Anasema alama ni chombo au mashine au rangi iliyopakwa au kutokupakwa ili kuweza kutoa picha au ujumbe wa mazingira ya eneo alipo mtumiaji wa barabara.
Ujumbe huo unaweza kuwa ni kiwango cha mwendo wa juu kinachoruhusiwa katika barabara husika, ama sehemu ambayo dereva anatakiwa kuwaacha watumiaji wengine wa barabara wavuke kwanza na ni maeneo ambayo mtumiaji hupata huduma zingine, kama vile za mafuta ya petroli au dizeli.
Anasisitiza kuwa mtu hawezi kuwa dereva bila ya kuwa mahiri kwenye tafsiri sahihi za alama za michoro ya barabarani na kuzitekeleza kwa wakati mwafaka.
Ukurasa wa 2 hadi wa 15, mtunzi anaelezea umuhimu wa lugha ya makundi ya alama za barabarani, ambapo anazitaja baadhi ya alama za makundi hayo kuwa ni alama za onyo na tahadhari, alama ya amri (amri zinazokataza na kulazimisha), alama za taarifa na maelekezo na alama za usuli wa michoro ya barabarani.
Alama za usuli, hutoa tafsiri kadhaa zikiwemo zile zinazoonesha barabara kufungwa, ambapo rangi ya njano na nyeusi hutumika kuonesha kwamba barabara imefungwa kwa muda. Zipo pia alama za rangi nyekundu na nyeupe ambazo huonesha barabara kufungwa moja kwa moja na hivyo haiwezi kutumiwa na vyombo vya usafiri.
Alama zingine ni zile zinazoonesha dereva kutakiwa kupinda kulia au kushoto, zinazoonysha kona kali iliyo kwenye barabara husika na nyinginezo nyingi. Msomaji anashauriwa kununua kitabu hicho ambacho kinauzwa kwa Sh 7,000 na kinapatikana katika vyuo vya Veta vilivyo kwenye kanda zote na mikoa nchini.
Jambo zuri katika kitabu hicho alama zote zimeorodheshwa na kuwekewa tafsiri yake, jambo ambalo litamuwezesha msomaji kukisoma kitabu hicho na kukielewa vizuri. Ukurasa wa 16 wa kitabu hicho, mtunzi anawaonesha askari wa Usalama Barabarani, wanavyotakiwa kutoa amri kwa watumiaji wa barabara, ambapo ishara mbalimbali kuhusiana na maaskari wanavyotakiwa kusimama na kutoa amri hizo zimefafanuliwa katika kitabu hicho.
Ukurasa wa 17 mtunzi anaelezea juu ya alama za barabarani, onyo na taarifa kwa makundi maalum zinazokwenda sanjari na tafsiri za alama za taarifa kwa makundi maalum.
Makundi hayo ni ya watu wa ulemavu tofauti tofauti katika jamii. Kwa mfano, mtunzi anaonesha katika alama hizo kuwa mbele kuna kivuko cha walemavu wa macho, ama rangi ya fimbo inayotumiwa na walemavu wa macho mara kwa mara huwa ni ya rangi nyeupe.
Maelezo mengine aliyoeleza mtunzi ni utunzaji wa gari, usafishaji wake, uwekaji wa vilainishi muhimu vinavyohitajika na kiwango cha joto. Pia kuna taasisi zinazojihusisha na kuangalia ubora wa oili, ambapo hapa dereva anashauriwa kuwa na utaratibu wa kutumia oili yenye mchanganyiko wa hali ya hewa.
Mengine ni vigezo vya kuangalia wakati wa kununua oili, namna ya kutumia mafuta ya breki, muda wa kufanya kazi kwa magurudumu, ambapo dereva anashauriwa kutumia aina ya mafuta ya breki yaliyopendekezwa na mtengenezaji wa gari kama ambavyo husomeka kwenye mfuniko wa mtungi wa mafuta ya breki!
Mtunzi anahitimisha kwa kumtaka, dereva aendeshe gari lake kwa kuzingatia taarifa zilizopo kwenye tairi, asibebe mzigo kupita kiasi, asiweke tairi lililo na mwendokasi tofauti na mwendokasi unaozalishwa kwenye injini, tairi lisilo kuwa na uwezo wa kuhimili matope kwenye barabara za tope nyakati za mvua.
Ni imani kwa watu wengi kwamba madereva wa pikipiki wataacha ubahili na kuwa wa kwanza kununua kitabu hiki kwani wengi wanaendesha bila kujua ama kufuata kanuni za usalama barabarani. Imani pia ni kwamba, kwa vile elimu haina mwisho, hata madereva ambao tayari wamepita vyuoni na wako barabarani watachangamkia kitabu hiki ili kujenga utamaduni wa kujikumbusha kile walichojifunza mara kwa mara.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family